Mchango wa Kihindi katika Leksikografia ya Kiswahili
Abstract
Leksikografia ya Kiswahili sanifu imewahi kuimarishwa na lugha nyinginezo za kigeni: Kiajemi, Kiarabu, Kiibrania, Kichina, Kifaransa, Kigiriki, Kihispania, Kijerumani, Kijapani, Kilatini, Kiingereza, Kituruki, Kireno na Kihindi. Lugha hizi zimechangia kiasi kikubwa uundaji wa vidahizo katika kamusi mbalimbali za lugha ya Kiswahili ikiwemo Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Tafiti kuhusu michango ya baadhi ya lugha hizi zimefanywa na wataalamu kuhusu Kiingereza na Kiarabu; hata hivyo lugha ya Kihindi haijashughulikiwa licha ya kwamba imechangia leksimu anuwai katika kamusi za Kiswahili sanifu. Hivyo basi, makala haya yanaangazia mchango wa lugha ya Kihindi katika leksikografia ya Kiswahili ili kubaini leksimu zilizokopwa moja kwa moja au kukopwa kwa kutoholewa na hatimaye kuingizwa katika Kiswahili sanifu. Ili kufanikisha dhamira hii, makala yamehusisha historia ya Wahindi katika Afrika Mashariki, yameangazia baadhi ya misamiati iliyokopwa moja kwa moja na kwa kutoholewa kwa kurejelea Kamusi ya Kiswahili Sanifu Toleo la 3 kama matini maalumu, kurejelea maumbo ya maneno asilia ya Kihindi yaliyokopwa na kuingizwa katika Kiswahili, na hatimaye kufafanua ruwaza iliyozingatiwa katika ukopaji wa kiutohozi wa maneno hayo kutoka Kihindi hadi Kiswahili. Makala haya yamechangia kijimada kuhusu leksikolojia na leksikografia ya Kiswahili.