Taarifa kwa Waandishi wa Makala

Uandaaji na Utumaji wa Makala

Jarida linapokea makala yaliyoandikwa kwa Kiswahili TU. Makala yapigwe chapa katika muundo wa Microsoft Word, mstari ikitengwa kwa kipimo cha nafasi ya 1.5 baina ya mstari na mstari na pambizo liwe na upana toshelevu. Ukurasa wa kwanza wa makala uoneshe jina la makala, jina kamili la mwandishi (au waandishi) wa makala (ikiwa ni pamoja na wadhifa wake) na anwani yake na baruapepe. Ukurasa wa pili uoneshe jina la makala na ufupisho wa makala (Ikisiri) kwa maneno yasiyozidi 300. Makala yawe na ukubwa wa maneno kati ya 3000-8000 na mapitio ya vitabu maneno 700-1200.

Upitiaji na Uhariri wa Makala

Makala yoyote kabla ya kuwasilishwa yawe yamepitiwa vema na mwandishi na kufanyiwa uhariri wa kina kuhakikisha kwamba makala hayana makosa ya kiundishi na kimaudhui. Mwandishi anapaswa pia kuhakikisha kwamba taarifa zote zilizomo ndani ya makala ni sahihi na vyanzo vya taarifa hizo ni vyenye kuaminika.

Urejeleaji

Unapotaja marejeleo kwenye matini taja jina la mwisho la mwandishi, likifuatiwa katika mabano na tarehe ya chapisho lake na kurasa zilizorejelewa, k.m. Yahya (1983:139). Kwenye orodha ya marejeleo au bibliografia majina ya warejelewa yapangwe kialfabeti. Tanchini na tanmwisho ziwekwe namba na zitumike pale tu inapobidi. Maelezo ya tanimwisho yatolewe kwenye ukurasa wa pekee mwisho wa makala, yaani kabla ya kuorodhesha marejeleo.

Majina ya vitabu na majarida yaandikwe kwa italiki, anwani za tasnifu/tazmili ziandikwe bila italiki wala kuweka alama za kufunga na kufungua semi, na majina ya makala yawekwe ndani ya alama za kufunga na kufungua semi kama inavyoonekana katika mifano ifuatayo:

TUKI. (2013). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Nairobi: Oxford University Press.

Hamisi, A.M. (2008) “Filosofia za Sera za Lugha”. Katika J.G. Kiango (Mh.) Maendeleo ya Lugha. Dar es Salaam: TUKI. Kur. 78-100.

Chiraghdin, Sh. (1974) “Kiswahili na Wenyewe”.  Mulika, Juz. Na. 6: 35-41.

Omari, S. (2009) Tanzanian Hip hop Poetry as Popular Literature. Tasinifu ya Uzamivu (Haijachapishwa). Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mifano na Vielelezo ndani ya Makala

 

Mifano yote, majedwali, michoro, ramani na picha mbalimbali vipangwe kwa uwazi na unadhifu kwenye kila ukurasa kadiri vilivyotumika. Taarifa zote hizo zinapaswa kutumika kwa kuzingatia kanuni za maadili ya kazi ya kitaaluma. Mathalani, ni muhimu kuweka chanzo thabiti cha taarifa inayoingizwa kwenye makala, iwe ni picha, michoro, mifano na vingine vinavyohusiana na hivyo.

Udanganyifu wa Kitaaluma

Kunakili maneno, mawazo, michoro, n.k., kutoka vyanzo vingine bila kubainisha vyanzo husika kutatafasiriwa kuwa ni udanganyifu wa kitaaluma na hiyo inaweza kuwa miongoni mwa sababu za makala yako kukataliwa. Ikiwa itabainika kuwa makala yaliyochapishwa katika jarida yamekiuka maadili ya kazi za kitaaluma,  taratibu za kisheria zitachukuliwa kulingana na kanuni na miongozo iliyopo.

Ridhaa ya Kuchapisha

Ikiwa muswada utakubaliwa, mwandishi wa makala ataandikiwa barua kupewa taarifa hiyo. Mwandishi wa makala  atapaswa kuthibitisha kwa maandishi kwamba makala hayo hayajakusanywa wala kuchapishwa mahali pengine. Taarifa hiyo itachukuliwa kuwa ni idhini ya makala hayo kuchapishwa katika Jarida la Mulika.