Makala ya Mulika yatatathminiwa na wasomaji wasiopungua wawili ambao watafanya kazi hiyo bila kufahamu taarifa za mwandishi. Waandishi wanatakiwa kuepuka kuonesha utambulisho wowote unaowahusu ndani ya makala ili kuwawezesha wanaoitathmini kufanya kazi yao kwa haki. Sifa mojawapo ya watu watakaotathmini makala ni weledi katika uwanja unaofanyiwa tathmini. Makala yatapowasilishwa yatapitiwa kwanza na wahariri wa jarida ili kuhakikisha kwamba makala yametimiza mahitaji ya jarida kabla hayajatumwa kwa watathmini wa nje.
Endapo maudhui ya makala yatakidhi mawanda na sera za jarida, makala yatatumwa kwa watathmini wasiopungua wawili ambao hawajulikani na mwandishi, kuwaomba kukubali kuitathmini makala. Watathmini watatathmini miswada wakilenga kuangalia ubora wake katika maudhui, uwazi wa uwasilishaji, uasili, mchango wake kitaaluma na uzito wake kimaudhui na kiutafiti. Watathmini watapatiwa mwongozo utakaowaongoza wakati wa kutathmini makala. Baada ya kupata maoni ya watathmni wahariri watapitia maoni hayo kabla ya kuyatuma kwa waandishi wa makala ili kuhakikisha kwamba maoni yaliyotolewa yanaendana na mwongozo uliotolewa. Baada ya maoni hayo kupitiwa na wahariri kujiridhisha kwamba yanaendana na mwongozo wa jarida yatatumwa kwa waandishi wa makala ili waweze kuyafanyia kazi kisha kurejesha mswada uliozingatia maoni yaliyotolewa na watathmini wa makala.
Miongoni mwa vipengele vitakavyozingatiwa wakati wa kutathmini makala ni walengwa wa makala, lengo la makala, mapitio ya maandiko, nadharia, mpangilio na uwasilishaji, ufafanuzi wa maudhui, uasili na uzingatiaji wa maadili, matumizi ya michoro na picha, uandishi wa matini na marejeleo.
Kutokuzingatia mwongozo wakati wa kuandaa makala kunaweza kuwa sababu ya makala kutopewa nafasi katika hatua za awali za tathmnini. Aidha, kutokuzingatia makataa ya kufanya marekebisho kwa waandishi wa makala kunaweza kuwa sababu ya makala hayo kutokuzingatiwa katika toleo husika.
Waandishi ambao makala yao yatakubaliwa wataandikiwa barua kuwajuza hatua hiyo na baada ya jarida kutoka kila mwandishi atatumiwa nakala tepe ya makala yake kwa marejeleo.
Maoni yaliyomo kwenye jarida hili ni ya waandishi wa makala na si lazima yakubaliane na yale ya Wahariri au Kamati ya Uhariri ya Taasisi ya Taaluma za Kiswahili.