Ubeberu wa Kiisimu na Mustakabali wa Lugha za Kiafrika: Mapitio ya Sera ya Lugha Tanzania

Gervas A. Kawonga

Abstract


Makala haya yanahusu ubeberu wa kiisimu na mustakabali wa lugha za Kiafrika, Tanzania ikichukuliwa kama mfano. Ubeberu wa kiisimu (UK) ni mkabala wa kinadharia unaochunguza ikolojia ya kiisimu inayozifanya baadhi ya lugha kuthaminiwa na kutumika zaidi kuliko nyingine. Kupitia uchambuzi wa kiisimujamii hoja ya makala haya ni kwamba sera ya lugha inatishia ustawi wa lugha za jamii na kwa upande mwingine haiweki ustawi endelevu wa Kiswahili. Mapitio ya sera ya lugha ya Tanzania, kihistoria mpaka 2014, yanaonesha kwamba Kiswahili kina hadhi ya juu kuliko lugha zingine za jamii katika ikolojia ya kiisimu. Hata hivyo, hadhi ya Kiswahili haijawekewa kinga thabiti ya kuifanya kuwa endelevu kwa sababu sera iliyopo si madhubuti kiasi cha kukabiliana na tishio la ubeberu wa lugha ‘kubwa’ kama Kiingereza, Kifaransa, Kichina kutaja baadhi. Makala haya yanaongozwa na mkabala wa Ikolojia ya Kiisimu (IK). Mkabala huu una madai kuwa katika jamiilughaulumbi kama ilivyo Tanzania, uhusiano wa lugha unaweza kufananishwa na ule wa wanyama wa mwituni ambapo wanyama wenye nguvu hutumia nguvu zao kuwakandamiza na kuwaua wanyama wadogo. Katika muktadha wa wingi lugha msingi huo una maana kwamba lugha zenye hadhi ya juu hazitoi nafasi kwa lugha zenye hadhi ya chini kuweza kuendelezwa. Msisitizo wa makala haya ni kwamba ustawi wa Kiswahili na lugha za jamii nchini Tanzania na barani Afrika kwa jumla ni jambo linalopaswa kuongozwa na sera yenye kuleta utangamano katika muktadha wa wingi lugha. Makala haya yanapendekeza kuwa nchi za Afrika ziache tabia ya kuzikumbatia lugha zinazokwezwa kama msingi wa ustarabu, maarifa, ukwasi na teknolojia na kuzifisha lugha za asili. Hitimisho la makala haya ni kwamba juhudi za makusudi lazima zifanyike miongoni mwa wadau wa lugha za Afrika ili kuzilinda na kuzifanya ziwe endelevu katika muktadha wa tishio kubwa la UK. Sera thabiti na madhubuti ni msingi wa ustawi wa lugha za Kiafrika nyumbani na ughaibuni

Full Text:

PDF

Refbacks

  • There are currently no refbacks.