Majina ya Wahusika katika Fasihi ya Kiswahili
Abstract
Makala hii inaangazia majina ya wahusika katika kazi za fasihi hususani fasihi ya Kiswahili kwenye utanzu wa riwaya. Inaonekana kwamba historia, imani na mazingira ya mwandishi ni miongoni mwa nduni zinazoweza kuchangia katika ujenzi na uteuzi wa majina ya wahusika katika kazi ya fasihi yoyote. Katika kuangalia mambo haya, makala imeangazia iwapo matukio yanaweza kujenga na kuteua majina ya wahusika kwenye kazi za fasihi. Kimahususi, uchunguzi unafanywa katika riwaya ya Dar es Salaam Usiku iliyoandikwa na Ben Mtobwa pamoja na riwaya ya Ua la Faraja iliyoandikwa na W. E. Mkufya. Nadharia ya semiotiki na elezi zimetumika katika uchanganuzi wa data kwenye riwaya teule kuangalia kama waandishi hao wameweza kujenga na kuteua wahusika katika kazi zao kulingana na matukio. Utafiti umebaini kuwa mitizamo ya kiimani, kikazi, kielimu, kikabila na kitabia imehusika katika ujenzi na uteuzi wa wahusika katika riwaya teule.