Dhima ya Ujozi Lugha katika Kufanikisha Mawasiliano: Mifano Kutoka Sajili ya Mchezo wa Kandanda
Abstract
Makala hii inanuia kuchunguza dhima ya ujozi lugha katika kufanikisha mawasiliano katika sajili ya mchezo wa kandanda. Lugha ni amali inayoamilishwa kutokana na mahitaji ya mawasiliano ya jamii. Matumizi ya lugha hutambuliwa na kubainika yanapoelekezwa na kudhibitiwa na kaida, maadili na mazoea ya jamii husika. Hata hivyo katika upekee wake, lugha huweza kukosa kukidhi mahitaji ya watumiaji wake katika nyanja zote za mawasiliano. Kwa hiyo, wakati mwingine lugha huhitaji au hulazimika kujiumbua na hata kuazima vipashio vya lugha nyingine ili kutimiza mahitaji haya mapya yanayoendelea kuchipuka nje ya mawanda ya kawaida. Kwa kuwa ni nadra kupata lugha inayojitosheleza, ujozi lugha hujitokeza kama mojawapo ya mbinu inayoziba ufa huu wa kimawasiliano katika matini bali si kama dhihirisho la umilisi mfinyu wa vipashio vya lugha husika.