Nafasi ya Kiswahili katika Mawasiliano ya Kijamii: Uchanganuzi wa Ujumbe Mfupi Unaosambazwa kwa Wagonjwa wa UKIMWI nchini Kenya
Abstract
Mawasiliano katika matibabu ni suala zito linalohitaji kushughulikiwa. Mawasiliano katika taaluma ya afya ni muhimu sana kwa kuwa yanaweza kuathiri pakubwa afya ya wanadamu na kuchangia maendeleo au pia kudumaza maendeleo. Kupokelewa na kusambaa kwa simu za kiganjani katika nchi ya Kenya, Afrika na ulimwenguni kote kumechangia maendeleo si haba katika teknolojia ya mawasiliano. Makala haya yanafafanua umuhimu wa kutumia Kiswahili katika ujumbe mfupi wanaosambaziwa wagonjwa wa UKIMWI, Kenya, chini ya mradi wa kimajaribio wa WelTel. Lengo kuu la mwandishi wa makala haya ni kuonesha kuwa wataalamu wa kimatibabu hawawezi kutoa huduma za kiafya kwa njia yenye ufanisi iwapo mawasiliano baina yao na wagonjwa yanakumbwa na vikwazo vya kimawasiliano. Kikwazo kimojawapo kwa mawasiliano hayo na ambacho kina athari kubwa ni lugha inayotumiwa. Jumbe zinazosambaziwa wagonjwa hawa kuhusu vyakula bora, dawa za kudhibiti maambukizi na makali husambazwa kwa lugha ya Kiingereza. Ni jambo la welekea kueleza kwamba lugha inayotumiwa na watu vijijini huwa ni lugha za asili. Aidha, asilimia kubwa ya wananchi wa Kenya wana ujuzi wa Kiswahili ambayo ni lugha ya taifa na rasmi. Isitoshe, Kiswahili ni lugha ya kibantu zao la jamii ya kiafrika na ni sehemu muhimu ya utamaduni wa kiafrika.
Maneno/ Dhana muhimu: Kiswahili, Kenya, teknolojia, ujumbe mfupi, mawasiliano ya kijamii, simu ya kiganjani, huduma za afya