Wahusika, Uhusika na Mtazamo katika Riwaya ya Kiswahili
Abstract
Wahusika ni kiungo muhimu katika utunzi wa riwaya. Wao ndio hubeba dhamira za mtunzi. Hii ina maana kwamba uchaguzi wao, majina wanayopewa na uhusika wao sharti vitekelezwe kwa ustadi mkubwa ili kufaulisha dhamira za mtunzi. Katika utunzi wa riwaya ya Kiswahili, tumeshuhudia maendeleo na mabadiliko katika namna wahusika wanavyo- sawiriwa. Njia ya moja kwa moja ya kuwatambulisha wahusika ni kuwapa majina ili yawe kitambulishi chao. Kisha kupitia kwa matendo yao tunaweza kujenga picha kuwahusu. Hii ndiyo njia rahisi na ambayo imetawala utunzi wa riwaya kwa kipindi kirefu. Hata hivyo watunzi wa riwaya ya Kiswahili ya kisasa wameonyesha maendeleo makubwa katika matumizi ya wahusika na uhusika katika kazi zao. Baadhi ya watunzi wametumia wahusika wao ili kuwasilisha mitazamo walio nayo. Watunzi kama hawa huchagua wahusika wao kwa uangalifu mkubwa kiasi kwamba tangu majina wanayowapa hadi wajibu wanaoutekeleza huwa ni mambo ambayo yameingiliana kiasi kwamba inakuwa rahisi kwa msomaji kutambua mitazamo na dhamira za mtunzi. Azma ya kazi hii ni kubainisha maendeleo ya aina hii ya usawiri na matumizi ya wahusika hasa majina yao. Tumetumia riwaya tatu kudhihirisha hili ambazo ni: Mafuta (Katama Mkangi), Vuta n ' kuvute (Shafi Adam Shafi) na Kosa la Bwana Msa (Muhammed Said Abdulla). Huu ni uchanganuzi matini ambapo kazi hizi pamoja na majina ya wahusika vimechaguliwa kwa kutegemea sampuli ya kimakusudi. Kazi hii imenuiwa kudhihirisha kuwa wahusika hawapewi majina ili kuwatambulisha tu bali majina hayo husheheni mitazamo ya watunzi na ndiyo yanayobeba maana na falsafa ya kazi ya riwaya. Uchanganuzi huu ni muhimu katika kuonyesha nafasi ya majina ya wahusika katika kuendeleza sanaa ya utunzi wa riwaya.
Dhana muhimu: wahusika, uhusika, mtazamo, maana, dhamira, ujumbe na riwaya