Ukiukwaji wa Nadharia Tumizi ya Uakifishaji katika Kazi za Kitaaluma za Wanafunzi wa Shule za Msingi Tanzania
Abstract
Makala haya ni zao la tasnifu ya Stephano (2015) yenye mada ya "Uzingatizi wa Viakifishi katika Uandishi wa Kitaaluma: Mifano kutoka Shule za Msingi Tanzania." Makala inabainisha misingi mikuu ya Nadharia Tumizi ya Uakifishaji na kuonesha ukiukwaji wake katika nyaraka zinazotumika kufundishia na kujifunzia Kiswahili katika shule za msingi. Data za utafiti huu zimetokana na mapitio ya nyaraka za kufundishia na kujifunzia Kiswahili. Nyaraka hizo ni vitini vya masomo ya wanafunzi wa Darasa la VI na VII, na vitabu vya kiada na viongozi vya walimu Darasa I - VII. Matokeo ya uchunguzi wetu yanaonesha kuwa Nadharia Tumizi ya Uakifishaji haizingatiwi kwa uhakika, hasa katika uandishi wa insha. Ni viakifishi vichache tu, nukta, kiulizo, mshangao (viakifishi vya Safu 1) na mkato (kiakifishi cha Safu 4) ikilinganishwa na idadi inayopendekezwa na nadharia (ambavyo ni viakifishi kumi na vinne), ndivyo vinavyotumika. Zaidi, matokeo yanaonesha kuwa, pamoja na kutumika, viakifishi hivyo havitumiki kwa usahihi. Kwa hiyo, makosa ya kuandika sentensi bebanifu, sentensi tata na vipande sentensi hutokea. Makala yanapendekeza Nadharia Tumizi ya Uakifishaji kuzingatiwa wakati wa kuandika ili kuandika matini zinazoeleweka kwa wasomaji.