Ujitokezaji wa Ruwaza ya Shujaa katika Ngano za Kiewe kutoka Ghana na Riwaya za Shaaban Robert kutoka Tanzania
Abstract
Fasihi imekubaliwa na wataalamu mbalimbali kuwa ni kioo cha jamii kwa kuwa inasawiri yale yaliyomo katika jamii. Kuna wataalamu wengine wanaoona kuwa kwa vile kila jamii ina utamaduni wake, hata kazi zao za fasihi zinatofautiana. Kwa upande mwingine, wapo wataalamu wanaoona kuwa jamii zenye mfanano mkubwa huweza kuwa na kazi za fasihi zinazohusiana. Wataalamu hawa wanaona kwamba, zaidi ya tofauti ndogondogo baina ya jamii hizo, mfanano ni mkubwa kwa kuwa msingi wa falsafa zao unafanana. Kwa mfano, wataalamu hawa huamini kuwa jamii nyingi za Afrika, ikiwamo Tanzania, zaidi ya tofauti ndogondogo miongoni mwao, zina mfanano mkubwa sana. Mfanano huo unaweza kubainika katika masuala mbalimbali kama vile falsafa, matumizi ya motifu mbalimbali, dhana ya ushujaa, mtazamo, fasihi na kadhalika. Hivyo, katika makala haya tunajiuliza, je, kuna mfanano baina ya ushujaa unaosawiriwa na masimulizi ya ngano ya Kiewe na riwaya teule za Shaaban Robert? Je, iwapo mfanano huo upo, unasawiriwaje katika kazi husika za fasihi? Kwa ujumla, makala haya yanakusudia kudadisi jinsi ushujaa unaosawiriwa katika jamii ya Waewe unavyotofautiana na kufanana na ule unasawiriwa katika riwaya teule za Shaaban Robert? Maswali haya yamejenga msingi wa makala haya kwa kutumia kiunzi cha Nadharia ya Ruwaza ya Shujaa iliyopendekezwa na Campbel (1973); Raglan (1979) na Kunene (1985). Aidha, makala haya yametumia ngano sita za Kiewe kutoka Ghana na riwaya mbili za Shaaban Robert kutoka Tanzania. Katika kazi hizo, mwandishi amechunguza namna ruwaza ya ushujaa inavyosawiriwa katika kumbo hizi mbili, yaani fasihi simulizi ya Waewe na fasihi andishi ya Waswahili.Downloads
Download data is not yet available.