Taswira na Mabadiliko ya Kiujumi katika Vitendawili vya Kiswahili
Abstract
Kwa kuwa fasihi haitokei katika ombwe, haiwezi kuepuka mabadiliko ya kiutamaduni, kifalsafa na kiujumi. Makala haya yanaangazia suala hili kwa kujikita katika utanzu wa fasihi simulizi, hususan vitendawili. Vitendawili vya Kiswahili kama sehemu ya fasihi, haviepuki athari za mabadiliko ya kiujumi yanayoikumba jamii ambamo vimeundwa. Mtazamo wa mwandishi wa makala haya ni kuwa thamani ya kiujumi iliyokuwamo katika vitendawili vya wakati uliopita pamoja na taswira zilizotumika nyakati hizo zina tofauti kubwa na zilizomo katika vitendawili vya sasa. Kadiri ulimwengu halisi unavyobadilika, tunatarajia pia kuwa thamani ya kiujumi inabadilika na hivyo taswira zinazotumika katika vitendawili zinabadilika ili kuendana na hali hiyo. Mawazo haya ndiyo kiini cha makala haya ambayo yamejikita kwenye mjadala unaohusu taswira na mabadiliko ya kiujumi katika vitendawili vya Kiswahili. Makala yana jumla ya sehemu tano zilizopangwa kama ifuatavyo: Sehemu ya kwanza ni utangulizi ambao unatoa picha ya jumla pamoja na kufafanua dhana za msingi kuhusu masuala yanayojadiliwa. Sehemu ya pili ni mapitio ya kazi tangulizi. Sehemu ya tatu inahusu methodolojia na nadharia ya utafiti. Matokeo ya uchambuzi yamebainishwa katika sehemu ya nne na sehemu tano ni hitimisho.