Taswira za Wanyama katika Mashairi ya Kezilahabi

Authors

  • Wael Nabil Ibrahim Othman Chuo Kikuu cha Al-Azhar

Abstract

Kezilahabi ni mhakiki na mtunzi maarufu wa ushairi, riwaya na tamthilia. Katika ushairi, ameandika diwani tatu ambazo ni Kichomi (1974), Karibu ndani (1988), na Dhifa (2008). Aidha, wahakiki wengi waliobobea katika fasihi ya Kiswahili wanaafikiana kwamba Kezilahabi ametumia kipengele cha taswira au picha katika kazi zake za kifasihi hasa katika mashairi yake kwa ufundi mkubwa. Miongoni mwao ni Senkoro (1988) anasisitiza kwamba ufundi wa taswira umezagaa katika diwani ya Kichomi iliyoandikwa na Kezilahabi, na kwamba shairi ambalo limetajwa na wahakiki wengi kuwa ni maarufu na ni kielelezo cha ufundi wa Kezilahabi katika matumizi ya taswira ni lile la "Nimechoka". Kadhalika, Saleh (1990) anafafanua kuwa picha ni kipengele muhimu sana katika mashairi ya Kezilahabi. Wamitila (1998) pia anaeleza kwamba Kezilahabi ni mwandishi ambaye yupo katika ngazi ya juu ya waandishi wanaomakinikia ujenzi tata wa ishara na taswira katika fasihi ya Kiswahili, kiasi kwamba ni vigumu kwa msomaji wa juujuu kufanikiwa kuziibua na kuzitafakari kwa kina mbinu zake. Kwa ujumla, maoni ya wahakiki waliowahi kuzichunguza kazi za Kezilahabi yanathibitisha kuwa kazi mbalimbali za kishairi zilizoandikwa na Kezilahabi zimesheheni matumizi makubwa ya taswira. Pamoja na mambo mengine, makala haya yanaendeleza mjadala wa matumizi ya taswira katika kazi za mtunzi huyu hasa kwa kuangazia dhana ya taswira, dhamira zinazoendelezwa na mtunzi kwa kutumia taswira husika pamoja na makundi au kategoria za taswira zijengwazo kwa kutumia wanyama.

Downloads

Download data is not yet available.

Downloads

Published

2021-08-17

Issue

Section

Articles