Mchango wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania katika Kueneza Kiswahili
Abstract
Kumekuwa na maandishi na machapisho mbalimbali ya Kiswahili yanayoonyesha mchango wa vyombo mbalimbali katika kueneza Kiswahili Tanzania na duniani kwa ujumla. Mchango huo mara nyingi umekuwa ukielekezwa katika vyama na asasi zilizoundwa kisheria kwa lengo la kukuza na kueneza Kiswahili nchini. Miongoni mwa vyama na asasi hizo ni Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI) ambayo ni zao la muunganiko wa Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) na Idara ya Kiswahili, zote za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA); Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA); Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU); Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki (CHAKAMA); Chama cha Lugha na Fasihi ya Kiswahili Tanzania (CHALUFAKITA) na asasi na vyama vingine vinavyofanana na hivyo. Mjadala kuhusu mchango wa asasi nyingine zisizojishughulisha na ukuzaji wa Kiswahili moja kwa moja ikiwa ni pamoja na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika kukuza Kiswahili haujajitokeza sana kwenye maandiko na mijadala ya kitaaluma. Hali hiyo siyo tu inaikosesha jamii taarifa muhimu juu ya ushiriki wa JWTZ katika kukuza lugha adhimu ya Kiswahili, bali pia inafinya fursa ya kupata marejeleo na fasili muhimu juu ya kazi kubwa inayofanywa na JWTZ kwenye muktadha huu. Makala haya yanaibua hoja na kuiweka mada hii hadharani ili jamii ipate kuelewa kwa kina mchango wa JWTZ kuhusiana na ushiriki wake katika kukiendeleza Kiswahili. Aidha, makala yatabainisha changamoto zinajitokeza kwa upande wa JWTZ katika kutekeleza jukumu hilo pamoja na mapendekezo ya namna ya kukabiliana na changamoto hizo JWTZ ili lizidi kukuza na kueneza lugha yetu adhimu ya Kiswahili.Downloads
Download data is not yet available.