Sababu za Matumizi ya Lugha Tandawazi katika Mtandao wa Facebook na Athari zake katika Kiswahili Sanifu
Abstract
Makala haya yamefafanua sababu za matumizi ya lugha tandawazi katika mtandao wa kijamii wa Facebook na athari zake katika Kiswahili sanifu. Data za makala haya zilitokana na kuwahoji watoataarifa kuhusu sababu za kutumia lugha tandawazi hususani katika mtandao wa kijamii wa Facebook. Vilevile, data zilitokana na upitiaji wa mawasiliano ya watu wanaotumia Kiswahili pamoja na lugha tandawazi katika mtandao wa Facebook. Makala yameongozwa na Nadharia Kidhi ya Mawasiliano (NKM) iliyoasisiswa na Howard Giles mwaka 1973. Matokeo ya utafiti huu yamebainisha kwamba watumiaji wa lugha ya mtindo huu hutumia lugha hii kwa malengo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kurahisisha mawasiliano na kuokoa muda pamoja na kuonesha ubunifu na upekee wa matumizi ya lugha. Vilevile, imebainika kwamba matumizi ya lugha tandawazi yana athari hasi katika Kiswahili sanifu kwa sababu hupotosha au huharibu sarufi na tahajia ya lugha ya Kiswahili sanifu kifonolojia, kimofolojia, kisitaksia, na kisemantiki. Aidha, kutokana na matokeo haya, mwandishi wa makala haya amependekeza kwamba watumiaji wa lugha tandawazi wawe makini katika matumizi ya lugha hususani katika miktadha rasmi kwa maana ya kwamba wasijisahahu kutumia lugha hiyo katika miktadha hiyo. Pia, vyombo vya kusimamia Kiswahili sanifu nchini vinashauriwa kukemea upotoshwaji/uharibifu wa lugha hiyo ambapo moja ya chanzo cha hali hiyo ni athari ya lugha tandawazi.