Athari za Masuala ya Kijamii kwenye Mfumo wa Ikolojia Jamii: Uchanganuzi wa Diwani za Bara Jingine na Rangi ya Anga
Abstract
Ikisiri
Makala haya yanalenga kuchunguza athari za masuala ya kijamii kwenye mfumo wa ikolojia jamii. Madhumuni ya uchunguzi huo ni kubainisha athari za masuala ya kijamii kwenye mfumo wa ikolojia kwenye diwani za Bara Jingine (Mberia, 2001) na Rangi ya Anga (Mberia, 2014). Aidha, ili kufanikisha azma hiyo, tumetumia mbinu ya usampulishaji lengwa katika kuchagua kazi ambazo zitatoa data mwafaka na kuzichanganua kwa njia ya maelezo huku tukitoa ufafanuzi na uthibitisho kutoka katika diwani ya Bara Jingine na Rangi ya Anga. Kadhalika, tumeongozwa na Nadharia ya Mfumo Ikolojia ambayo inaangazia uhusiano, upatano na mwingiliano kati ya binadamu na binadamu mwenzake au baina yake na viumbe wengine (Bronfenbrenner, 1989). Matokeo yaliyopatikana baada ya kufanyika kwa uchunguzi yamedhihirisha kuwa masuala ya kijamii kama vile matumizi ya mihadarati, ubaguzi wa kijinsia, ndoa za mapema na teknolojia ya kisasa yanaathiri mfumo wa ikolojia. Hii ni kwa sababu maisha ya binadamu na viumbe wengine hayawezi kukamilika bila kutegemeana. Isitoshe, kuingiliana na kutagusana baina ya binadamu mmoja na mwingine kunaibua migogoro na mikinzano ambayo huathiri si ustawi wa binadamu pekee, bali pia ustawi viumbe wengine. Hii ni kwa kuwa wote wanaishi kwenye mazingira yaleyale. Tafiti za baadaye zinaweza zikashughulikia jinsi masuala ya kisiasa yanavyoathiri mfumo wa ikolojia.