Asili, Matumizi, na Mtazamo wa Salamu ya "Shikamoo" katika Jamii ya Watumiaji wa Lugha ya Kiswahili
Abstract
Ikisiri
Shikamoo ni moja ya salamu zinazotumiwa na jamii ya watumiaji wa lugha ya Kiswahili kusalimiana. Watu mbalimbali katika majukwaa tofautitofauti wamekuwa wakijadiliana kuhusu salamu hiyo endapo inawafaa watumiaji wa lugha ya Kiswahili au la. Makala haya yanajadili asili, matumizi, na mtazamo wa shikamoo wa jamii mbalimbali zinazotumia Kiswahili. Data za makala haya zimetokana na njia nne: upitiaji wa nyaraka, hojaji, usaili, na ushuhudiaji. Nadharia ya Ethnografia ya Mawasiliano (EM) imetumika kuongoza utafiti huu. Matokeo ya makala haya yanabainisha kwamba asili ya neno shikamoo ni: "nashika miguu" ambayo inaweza kuwa na fasili kuwa "nipo chini ya miguu yako". Asili hii ya neno shikamoo inanasibishwa na utumwa na ukoloni; inatajwa kuwa ni salamu iliyotumiwa na watwana kuwasalimia mabwana wao wakati wa ukoloni. Matumizi ya salamu hii kwa sasa kama ambavyo imebainishwa pia katika miongozo ya Kiswahili sanifu, ni salamu ya heshima kutoka kwa mtu mdogo kiumri kwenda kwa mkubwa. Aidha, utafiti huu umebaini kwamba 51% ya watumiaji wa lugha ya Kiswahili walioshiriki katika kujaza hojaji walidai salamu ya shikamoo ni nzuri wakati 30% walisema kuwa salamu hiyo ni mbaya kwa sababu ina asili ya utumwa/ukoloni na 19% walitoa majibu mengine yakiwemo kuiona salamu hiyo ina mapokeo mazuri na mabaya miongoni mwa watumiaji wa Kiswahili. Makala yanatoa rai kwamba ijapokuwa watu wengi wanapendezwa na salamu ya shikamoo, hatutakiwi kupuuza mawazo ya wale wanaoona salamu hiyo si nzuri; hivyo, inapendekezwa kwamba salamu hiyo isilazimishwe bali watu waitumie kwa hiari yao.