Kategoria za Maneno zenye Sinonimu za Asili na za Mkopo katika Kiswahili
Abstract
Ikisiri
Ukopaji wa maneno katika lugha ni mbinu mojawapo ya lugha kujitajirisha kimsamiati. Kuwapo kwa maneno ya mkopo katika lugha husababisha lugha kopaji kuwa na msamiati changamani, yaani msamiati wa asili na wa mkopo. Lugha inapokuwa na msamiati changamani hutokea wakati neno la asili linakuwa na kisawe kutoka lugha ngeni moja au zaidi, hivyo, kuibua sinonimu za asili na za mkopo, yaani neno moja ni la asili na lingine/mengine ni ya mkopo. Baadhi ya wataalamu kama vile Sarma, Bharali, Mahanta, Sakia na Sarmah (h.t); Kreidler (1998), Gelderen (2002), Griffith (2006) pamoja na Khamisi (2014) wanaeleza kuwa sinonimu katika lugha hujidhihirisha katika kategoria mbalimbali za maneno. Wataalamu hao wanaendelea kudai kuwa kati ya kategoria hizo zipo zenye sinonimu nyingi na nyingine zina sinonimu chache. Lugha ya Kiswahili inadhihirisha sifa ya kuwa na maneno ya asili na ya mkopo kutokana na kukopa maneno mengi kutoka lugha za kigeni (Chuwa, 1988; Besha, 1995; Kiango, 1995; King ' ei, 2010; Matinde, 2012). Kuwapo kwa maneno ya mkopo kunasababisha lugha hii kuwa na msamiati changamani, na hivyo, kuwa na sinonimu zenye asili tofauti. Sinonimu hizo, kama ilivyoelezwa, zinajitokeza katika aina mbalimbali za maneno. Licha ya kujitokeza katika kategoria mbalimbali za maneno, bado suala hili halijawa wazi sana katika lugha ya Kiswahili hususani kategoria zenye sinonimu pamoja na kiwango cha ujitokezaji wa sinonimu katika kategoria hizo. Kwa hiyo, makala haya yanahusu kategoria za maneno zenye sinonimu za asili na za mkopo. Data za makala haya zimekusanywa kutoka matini za kamusi ambazo ni Kamusi ya Visawe (KV) (2014), Kamusi Kuu ya Kiswahili (KKK) (2017) na Kamusi ya Kiswahili Sanifu (KKS) (2019). Data zilizokusanywa zimechambuliwa kwa kutumia mbinu ya uchambuzi wa data kimaudhui na kiulinganishi. Ufafanuzi na ufasiri wa data zilizotumika umeongozwa na misingi ya Nadharia ya Vijenzi Maana.