Athari ya Mazingira Asilia ya Mtunzi katika Matumizi ya Kujibadilisha Kimazingaombwe: Uchunguzi wa Riwaya Teule za S. Robert na E. Kezilahabi
Abstract
Ikisiri
Makala haya yalikusudia kuchunguza athari ya mazingira asilia ya mtunzi katika matumizi ya kujibadilisha kimazingaombwe. Ili kulifikia lengo hilo, makala yameangazia jinsi mazingira asilia ya watunzi wawili yaani, Shaaban Robert na Euphrase Kezilahabi yalivyoathiri suala la matumizi ya mbinu ya kujibadilisha kimazingaombwe. Kazi za Shaaban Robert zilizoteuliwa ni riwaya za Adili na Nduguze (1952) na Kufikirika (1946) na kazi za Euphrase Kezilahabi zilijumuisha riwaya za Nagona (1990) na Mzingile (1991). Kujibadilisha kimazingaombwe ni mbinu ya kisanaa inayoonekana kuwa mashuhuri katika kazi za kifasihi za mihula mbalimbali. Mathalani, mbinu hii inapatikana siyo tu katika kazi za kifasihi zilizojitokeza katika kipindi cha usasabaadaye, bali pia mbinu hii inaonekana hata kwenye kazi za kale zaidi, hususani kipindi cha kabla ya usasabaadaye. Kutokana na usuli huo, riwaya za Shaaban Robert zilizoteuliwa zimewakilisha kipindi kabla ya usasabaadaye ilhali riwaya za Kezilahabi ni za kipindi cha usasa na usasabaadaye. Tumechagua riwaya zilizoandikwa katika vipindi hivyo tofauti ili kuthibitisha kuwa mbinu ya kujibadilisha kimazingaombwe ni ya kale, ilikuwako hata kabla ya kipindi cha usasabaadaye. Matokeo yanaonesha kwamba tafsiri ya dhana au wazo katika kazi ya kifasihi imefungamana mno na muktadha wa kijamii uliozaa kazi hiyo. Kutokana na athari ya muktadha wa kijamii, dhana, wazo, suala au tukio fulani linaweza kuonekana la kimazingaombwe katika kazi ya kipindi fulani ilhali dhana, wazo, suala au tukio hilohilo linaweza kuonekana kuwa la kawaida (lisilo la kimazingaombwe). Mabadiliko hayo yanaweza kusababishwa na maendeleo ya sayansi na teknolojia au na maingiliano ya jamii kiutamaduni na kiimani. Kwa kuongozwa na mtazamo huu, kujibadilisha kimazingaombwe kumebainishwa katika riwaya teule na kisha imeelezwa jinsi ujitokezaji wa mbinu hii ulivyofungamana na uhalisia wa maisha ya wanajamii kadiri ya mazingira asilia yaliyowazaa, kuwalea na kuwakuza watunzi wa riwaya teule.