Umuhimu na Changamoto za TEHAMA katika Ufundishaji na Ujifunzaji wa Lugha ya Kiswahili kwa Wageni

Authors

  • Sarah Vicent University of Dar es Salaam
  • Arnold B. G. Msigwa

Abstract

Ikisiri

Ulimwengu wa utandawazi umesababisha kusambaa kwa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), hususani matumizi ya kompyuta na viambata vyake. Kwa hali hiyo, maendeleo yamesababisha kuenea kwa lugha zinazotumika katika teknolojia hiyo kama vile Kiingereza na lugha nyingine za Kimagharibi, na kwa kiasi kidogo, lugha za Kiafrika kama vile Kiswahili. Hata hivyo, TEHAMA imekuwa ikitumiwa na walimu na wanafunzi katika kufundishia na kujifunzia lugha za kigeni hasa Kiingereza kama inavyoelezwa na Lopez (2016), Bostina (2016), Bilyalova (2016). Aidha, zipo tafiti chache zilizozungumzia changamoto za kutumia Kiswahili katika TEHAMA, kwa ujumla, bila kuzungumzia namna Kiswahili kinavyoweza kutumika kiteknolojia katika ufundishaji na ujifunzaji kwa wageni. Kwa hiyo, makala haya yamejadili suala hilo na yanajikita katika kufafanua umuhimu na changamoto za TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji wa Kiswahili kwa wageni. Aidha, makala haya yametoa mapendekezo ya nini cha kufanya ili kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika ufundishaji na ujifunzaji huo. Data zilizotumika katika makala haya zimepatikana kwa njia ya dodoso. Mkabala wa kitaamuli umetumika katika kuchambua data. Matokeo yamebaini kuwa kuna umuhimu wa kutumia TEHAMA katika kufundishia na kujifunzia Kiswahili kwa wageni kwani inarahisisha ufundishaji kwa maana ya kutumia muda mfupi kufundisha mambo mengi. Pia, inamfanya mwanafunzi afurahie somo bila kuchoka na kupunguza gharama za ujifunzaji. Pamoja na umuhimu huo, zimebainika changamoto katika matumizi ya TEHAMA, yaani wakati mwingine wanafunzi wanapata shida kutumia matini zilizo mtandaoni kutokana na kukosa mwingiliano wa moja kwa moja na mwalimu, kukosekana kwa matini za kutosha na zilizoandikwa kwa usahihi mitandaoni, kukosekana kwa vifaa kama projekta na kompyuta na baadhi ya walimu na wanafunzi kutokuwa na maarifa ya kutosha ya matumizi ya vifaa hivyo. Kwa ujumla, makala yanahitimisha kwamba upo umuhimu wa kupendekeza mbinu zinazoweza kukabiliana na changamoto hizo kama vile kuwa na semina za mara kwa mara za kufundisha namna ya kutumia vifaa vinavyohusiana na TEHAMA, kuwa na vifaa vya kutosha na vinavyokidhi mahitaji ya ufundishaji na ujifunzaji wa Kiswahili kwa wageni kwa kutumia TEHAMA kwenye taasisi za watu binafsi na taasisi za serikali.

Downloads

Download data is not yet available.

Downloads

Published

2022-04-16

Issue

Section

Articles