Ukuzaji wa Stadi ya Tafakuri Bunifu kupitia Ufundishaji wa Fasihi: Mfano wa Shule Teule Nchini Rwanda
Abstract
Tafakuri bunifu ni miongoni mwa stadi za karne ya ishirini na moja zinazotajwa kuwa muhimu hususani katika kusaidia kutatua tatizo la uhaba wa wafanyakazi wanaokidhi mahitaji ya soko la ajira (Urban, 2007). Licha ya hivyo, tafiti zinaonesha kwamba kiwango cha tafakuri bunifu miongoni mwa wanafunzi kingali kidogo na hivyo kuathiri sana mafanikio ya sekta ya elimu (Jack, 2013). Kutokana na hali hii, tuliona ni muhimu kufanya utafiti kuhusu ukuzaji wa tafakuri bunifu kupitia ufundishaji wa fasihi. Makala haya yalikuwa na malengo matatu: mosi, kuchunguza nafasi ya fasihi katika ufundishaji wa tafakuri bunifu; pili, kuchunguza namna ambavyo walimu wa fasihi hujumuisha stadi ya tafakuri bunifu katika maandalio ya masomo, ufundishaji, na tathmini; na mwisho, kuunda mwongozo wa ufundishaji wa tafakuri bunifu kupitia fasihi. Ili kutimiza malengo haya, mbinu ya ushuhudiaji, uchanganuzi wa matini na usaili zilitumiwa. Data zilichambuliwa kwa madondoo na maelezo. Aidha, makala haya yaliongozwa na Nadharia ya Utambuzi katika hatua za ukusanyaji, uchambuzi na uwasilishaji wa data. Licha ya matokeo ya utafiti kuonesha kuwa fasihi ina nafasi muhimu katika ufundishaji wa tafakuri bunifu, baadhi ya walimu hawafanikiwi kujumuisha stadi ya tafakuri bunifu siyo tu katika maandalio ya masomo, bali pia katika ufundishaji na tathmini. Ikiwa ni sehemu ya kukabiliana na vikwazo hivyo, matokeo ya utafiti yamebainisha mwongozo unaopaswa kufuatwa na walimu katika ufundishaji wa stadi za tafakuri bunifu kupitia fasihi.