Fonolojia ya Nomino na Vitenzi katika Kimochi
Abstract
Makala haya yamelenga katika kufafanua vipengele anuwai vya fonolojia vipande sauti vya lugha ya Kimochi. Miongoni mwa vipengele vya kifonolojia vilivyoangaziwa ni irabu, konsonanti, muundo wa silabi, na michakato ya kifonolojia kwa kutumia nadharia ya vipande sauti Huru, iliyoasisiwa na Chomsky na Halle (1968). Data zilizotumika zimekusanywa uwandani katika vijiji viwili vya Mori na Mbokomu vilivyo katika wilaya ya Moshi vijijini, mkoa wa Kilimanjaro. Kama ilivyo katika lugha nyingi za Kibantu, imeonekana kwamba Kimochi kina jumla ya irabu tano (5) na konsonanti thelathini na moja (31) na kwamba michakato mbalimbali inayojitokeza katika Kimochi ni majumui. Hivyo makala haya yatasaidia kwa wanaisimu linganishi kuona mfanano wa vipengele vilivyoshughulikiwa humu na vile vinavyojitokeza katika lugha nyingine za kibantu.