Utangamano baina ya Lugha ya Kiswahili na Lugha ya Kinyambo Kimofolojia: Uchambuzi wa Maeneo Mahususi
Abstract
Lengo la makala haya ni kuonesha utangamano wa lugha ya Kiswahili na lugha ya Kinyambo. Utangamano wa lugha hizo umeoneshwa katika baadhi ya vipengele vya kimofolojia ambavyo ni mbinu za uundaji wa maneno na katika utumizi wa baadhi ya viambishi. Data ya makala haya imepatikana kwa namna tofauti ambazo ni: mosi, katika orodha ya msamiati wa Kinyambo ili kupata maneno ya mkopo ya Kiswahili yanayotumika katika Kinyambo. Pili, maandiko ya wataalamu mbalimbali yamehusishwa ili kupata mifano ya maneno yenye viambishi maalumu vinavyoonesha utangamano katika lugha hizo. Tatu, ujuzi wa lugha hizi mbili alionao mwandishi wa makala haya umesaidia kupata na kuielewa data. Uchanganuzi wa data hizo umeongozwa na Nadharia ya Mofolojia Leksika ili kuonesha mipaka ya viambishi katika maneno. Uchanguzi wa data hizo umedhihirisha masuala yafuatayo: kwanza, katika uundaji wa maneno, maneno yenye vibadala vyake katika lugha ya Kinyambo yanakopwa tena kutoka Kiswahili. Hali hii imeonesha utangamano wa wazi kwa kuwa hakuna hitaji la msingi la ukopaji wa namna hiyo kutokana na kuwapo kwa vibadala vya maneno hayo katika lugha hiyo. Pili, pamoja na kwamba kuna viambishi ambavyo havikubaliki katika Kiswahili rasmi, watumiaji wa lugha ya Kiswahili wanavitumia katika mawasiliano ya kawaida. Hali hii inadhihirisha utangamano wa lugha hizo mbili kwa sababu viambishi hivyo vinatumika katika lugha zinazoingiliana sana na Kiswahili. Hivyo, kwa kuwa lugha hutangamana na kubadilika, uchambuzi wa maneno kimofolojia haupaswi kwenda mbali na mabadiliko hayo ili kuona namna maumbo ya maneno yanavyobadilika na yanavyotumika katika lugha husika ili kwenda na uhalisia ulivyo.