' Kifo ' cha Uhafidhina wa Maulidi: Athari za Utandawazi na Uchipukaji wa Ukanivali katika Sherehe ya Kidini Visiwani Lamu, Kenya
Abstract
DOI: https://doi.org/10.56279/mulika.na42t1.1
Sherehe za Maulidi ni maarufu katika kalenda ya Waswahili visiwani Lamu. Wageni kutoka pembe zote za dunia wamekuwa wakijumuika na wenyeji wakati wa sherehe hizi za kidini. Pale ambapo Al-Habib Swaleh Jamal Layl ' alipoanzisha ' sherehe hizi, ngoma kuu iliyochezwa ilikuwa uta. Hii ni ngoma ya wagema na watu wa tabaka la chini. Baadaye, kukaingizwa ngoma mbalimbali kama vile kirumbizi, hanzua, mdurenge, chama, Goma na Umm-al-Qura (Kasida ya Hamziyyah). Wakati huu wote, sherehe za Maulidi zilikuwa za kidini, na lengo kubwa lilikuwa kutukuza ' mazazi ' ya Mtume Muhammad. Sherehe hizi za Maulidi zimekuwa kama ' Haji toto ' kwa baadhi ya wanaoshiriki, hasa wale ambao hawangeweza kutimiza nguzo mojawapo ya Kiislamu ambayo ni kusafiri kwenda Makka ili kuhiji. Hata hivyo, katika vipindi hivi vya utandawazi, ambapo dunia imekuwa finyu na kuwa kama kijiji kimoja, visiwa vya Lamu vimejikuta katika njia panda iliyosababishwa na utandawazi huu. Sherehe za Maulidi ambazo awali zilikuwa za kidini, zimepitia mabadiliko makubwa kutokana na sababu mbalimbali za kiutandawazi. Limekuwa jambo gumu kuchora mpaka kati ya sherehe za kidini za kitamaduni za watu wa Lamu na sherehe za kikanivali. Makala haya yanalenga kutathmini mabadiliko katika sherehe hizi kwa muktadha wa utandawazi. Je, ni kwa namna gani mitandao ya kijamii ilivyochangia kutokea kwa mabadiliko haya?