Mabadiliko ya Kiuimbaji ya Nyimbo za Ibada katika Kanisa Katoliki Tanzania: Uchunguzi wa Makanisa Teule
Abstract
DOI: https://doi.org/10.56279/mulika.na42t1.2Makala haya yanahusu mabadiliko ya kiuimbaji ya nyimbo za ibada na athari zake katika Kanisa Katoliki, Tanzania. Makanisa mawili ya kikatoliki ya Dar es Salaam yalichunguzwa, Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu na Kanisa la Mtakatifu Paulo Mtume Ubungo-Msewe. Makanisa haya yalichaguliwa kutokana na kuwepo kwa wamisionari wageni na wazawa waliosaidia kupatikana kwa taarifa muhimu za utafiti uliofanyika. Njia zilizotumika kukusanya data ni utalii wa uwandani, mahojiano na majadiliano. Utafiti uliofanyika ulilenga kujibu maswali yafuatayo: ni mabadiliko gani ya kiuimbaji yaliyotokea katika nyimbo za ibada za kikatoliki Dar es Salaam? Ni mambo gani yaliyosababisha mabadiliko ya uimbaji wa nyimbo za ibada katika Kanisa Katoliki Dar es Salaam? Data zilizokusanywa zilichambuliwa kwa kutumia Nadharia ya Utendaji. Matokeo ya utafiti yalionesha kuwa yapo mabadiliko katika muktadha wa utunzi wa nyimbo, maudhui, lugha, na waimbaji wa nyimbo yaliyoleta uhuru wa kusali kwa Watanzania na kulijenga kanisa lao. Mabadiliko haya yalisababishwa na kupatikana kwa uhuru wa Tanzania Bara, Mtaguso wa Vatikano II, utamadunisho, biashara na kukua kwa sayansi na teknolojia Tanzania.