Changamoto za Kipragamatiki kwa Wanafunzi wa Kiswahili Nchini Rwanda
Abstract
DOI: https://doi.org/10.56279/mulika.na42t1.7
Makala haya yanalenga kuchunguza changamoto za kipragmatiki kwa wanafunzi wa Kiswahili nchini Rwanda. Ingawa wanafunzi Wanyarwanda wanajifunza lugha hii kuanzia mwaka wa kwanza wa shule za sekondari, imedhihirika kuwa wanapambana na changamoto mbalimbali katika matumizi yao ya Kiswahili (Ntawiyanga, 2015). O'Keeffe (2011) anafafanua kuwa ustadi wa kipragmatiki ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazowakabili wanaojifunza lugha na kuwa ni vigumu kuukuza uwezo huu kwa sababu maendeleo yake hayatokani na umilisi wa kisarufi. Makala haya yameweka bayana changamoto za kipragmatiki kwa wanafunzi wa Kiswahili nchini Rwanda, sababu au vyanzo vya changamoto hizo, na yametoa mapendekezo ya namna ya kukabiliana nazo. Utafiti huu umeongozwa na Nadharia ya Urekebishaji Mawasiliano ya Giles (1973) ambayo inaweka pamoja vipengele vya kisaikolojia na vya kijamii katika kuamua mtindo wa mawasiliano yenye mwingiliano au mtagusano wa kijamii. Mbinu zilizotumika kukusanya data za utafiti huu ni hojaji pamoja na mahojiano. Wanafunzi wa Kiswahili katika Ndaki ya Elimu, Chuo Kikuu cha Rwanda pamoja na wahadhiri wao ndio walioshirikishwa katika utafiti huu. Kulingana na uchunguzi wa data iliyotumika katika makala haya, imedhihirika kuwa wanafunzi wa Kinyarwanda hukabiliwa na changamoto ambazo hutokana na uhamisho wa mitindo ya lugha kutoka Kinyarwanda hadi Kiswahili. Aidha, imedhihirika kuwa vyanzo vingi vya changamoto hizi ni kujifunzia Kiswahili nje ya utamaduni wake, kutojali mtindo sahihi unaopaswa kutumiwa pamoja na ukosaji wa kielelezo cha kufuatilia.