Athari za Kimsamiati za Mtagusano wa Jamii-Lugha ya Waswahili na Jamii-Lugha Nyingine za Kigeni

Musa Mohamed Salim Shembilu

Abstract


DOI: https://doi.org/10.56279/mulika.na42t1.8

Kiswahili kimekuwa ni miongoni mwa lugha zinazokua kwa kasi ndani na nje ya Bara la Afrika. Katika kukua huko kimetagusana na jamii-lugha nyingine za kigeni kama vile Kiarabu, Kireno, Kijerumani, na Kiingereza. Zipo jamii-lugha zilizotagusana na Kiswahili kutokana na sababu za kiutawala kama vile Kiarabu, Kijerumani na Kiingereza. Zipo pia zilizotagusana kwa sababu za kijamii ambazo ni kama vile Kihindi na Kituruki. Makala haya yanajaribu kutalii mtagusano wa Kiswahili na jamii-lugha nyingine kwa lengo la kuona jinsi lugha hizi zilivyoathiriana kimsamiati. Mtagusano wa Kiswahili na jamii-lugha nyingine umesababisha kuibuka mitazamo mbalimbali kuhusu chimbuko na asili ya Kiswahili. Kuhusu chimbuko, wapo wanaodai kuwa Kiswahili kilianzia sehemu moja na kusambaa sehemu nyingine na wapo wanaodai kuwa Kiswahili kilichimbukia sehemu mbalimbali za upwa wa Afrika Mashariki. Ama kuhusu asili, upo mtazamo unaokiona Kiswahili kama lugha inayotokana na Kiarabu. Vilevile, upo mtazamo unaochukulia Kiswahili kama lugha chotara na upo mtazamo unaodai kuwa Kiswahili ni Kibantu. Sababu za kuzuka kwa mitazamo hiyo ni kuwapo kwa msamiati au miundo yenye asili ya lugha za kigeni katika Kiswahili. Kwa mujibu wa makala haya, kama ambavyo imedokezwa pia na Massamba (2017), kupatikana kwa msamiati mwingi wa kigeni katika Kiswahili haiwi sababu ya Kiswahili kuwa na asili ya lugha hiyo ya kigeni bali ni matokeo ya lugha kuathiriana zinapokutana. Lugha zinapokutana huweza kuathiriana katika viwango mbalimbali kama vile sauti, mofimu, msamiati na sarufi kwa ujumla. Lengo kuu la makala haya ni kubainisha athari za kimsamiati zinazotokana na mtagusano huo wa jamii-lugha ya Waswahili na jamii-lugha nyingine. Aidha, pale ilipobidi athari za kifonolojia zimejadiliwa katika baadhi ya maeneo. Data ya utafiti huu ni ya maktabani. Hivyo, mbinu ya kukusanyia data ya makala haya ni usomaji matini mbalimbali zinazohusu mtagusano wa Kiswahili na lugha nyingine.


Full Text:

PDF

Refbacks

  • There are currently no refbacks.