Uchimuzi wa Epistemolojia ya Wabantu kuhusu Ontolojia ya Mtu katika Riwaya za Shaaban Robert
Abstract
DOI: https://doi.org/10.56279/mulika.na42t2.4
Makala haya yanazitagusanisha dhana mbili za kifalsafa ambazo ni epistemolojia na ontolojia. Maudhui ya makala haya ni sehemu ya matokeo ya utafiti mpana uliofanyika mwaka 2012 hadi 2016 kuhusu uchimuzi wa epistemolojia ya Wabantu katika riwaya ya Kiswahili. Mtu kama kiini cha falsafa anatazamwa kwa namna tofauti kulingana na utamaduni, uzoefu au tajiriba za jamii husika. Hivyo, hoja ya msingi ya makala ni kuthibitisha kwamba Wabantu wana maarifa yao mahususi kuhusu wanavyomtazama mtu. Katika kuitetea hoja kuu ya makala, mjadala unajielekeza kwenye kujibu swali hili: ' Wabantu wanajua nini kuhusu kuwapo kwa mtu? ' Utafiti uliozaa makala haya uliongozwa na Nadharia ya Epistemolojia. Data zilikusanywa kwa kutumia mbinu za usaili na uchambuzi wa maandiko. Matokeo ya utafiti yanaonesha kwamba Wabantu wanambainisha mtu kwa vigezo vitatu ambavyo ni moyo wake, jina lake, na ardhi yake. Ithibati za hoja hizi zimetolewa katika riwaya tatu za Shaaban Robert, yaani, Kusadikika (2015), Kufikirika (2015), pamoja na Adili na Nduguze (1956).