DHIMA YA MWINGILIANOTANZU KATIKA SHEREHE ZA MWAKA KOGWA
Abstract
Makala hii inahusu umuhimu wa mwingilianotanzu katika fasihi simulizi ya Kiafrika kwa kutumia mfano wa miviga ya mwaka kogwa. Utafiti ulitumia miviga ya mwaka kogwa kama mfano wa jukwaa linalotoa fursa ya kudhihirisha mwingilianotanzu katika fasihi simulizi ya Kiafrika. Madhumuni ya makala hii ni kuonyesha namna ambavyo mwingilianotanzu huamilisha miviga ya mwaka kogwa. Imebainika kuwa, miviga ya mwaka kogwa hujengwa na kuamilishwa kutokana na uchanganyikaji wa tanzu zinazoingiliana kikorasi na kimatini, kutenguana, kujinyambua na kusemezana wakati wa utendaji. Mahusiano haya kati ya tanzu hizi ndani ya mwaka kogwa husaidia miviga hii kutekeleza wajibu wake kupitia njia anuai. Matokeo ya utafiti huu yamethibitisha maoni ya Senkoro (2011), aliyedai kuwa, inawezekana kabisa kuwa, tanzu za fasihi simulizi hazipaswi kuainishwa moja moja. Utafiti ulifanywa katika kisiwa cha Zanzibar na uchanganuzi ukafanywa kwa mujibu wa malengo ya utafiti. Mbinu ya Uchunzaji-Mahuluti inayojumuisha kushiriki, kushuhudia na kuhoji ilitumika katika kukusanya nyimbo, majigambo, malumbano ya utani na maghani, zikiwa tanzu kuu zilizowasilishwa wakati wa sherehe za Mwaka Kogwa, mwaka wa 2016. Kimsingi, utafiti huu umethibitisha kuwa, miviga ya mwaka kogwa ni mfumo timilifu wa maarifa, ambao unajengwa kutokana na mchanganyiko wa tanzu na vipera visivyoweza kutenganishwa katika hali halisi ya utendaji. Mchanganyiko huu wa tanzu ndio huiwezesha kutekeleza majumu yake mbalimbali miongoni mwa Wamakunduchi. Haya ni kinyume na mkabala uliopo unaopania kutenganisha fasihi simulizi katika tanzu zinazojitegemea (Bayo 2012, Okporoboro 2006, Ogumbiyi 1988 na Kubik 1977). Kwa hivyo, utafiti huu unaboresha mbinu za uainishaji na uchanganuzi wa fasihi simulizi ya Kiafrika kwa kuzingatia sifa ya mwingilianotanzu.