LUGHA NA UBONGO: ATHARI ZA KISAIKOLOJIA KATIKA KUIBUA MITINDO YA MATUMIZI YA LUGHA
Abstract
Lugha ni mfumo ambao ni tata sana katika maisha ya mwanadamu. Ni mfumo unaobeba maana halisi ya sauti anazotoa binadamu lakini pia hutumiwa na watu katika kuwasiliana. Lugha huweza kutumiwa na binadamu kwa namna mbalimbali na mitindo mbalimbali. Mtindo wa lugha humfanya binadamu kumfasili binadamu mwingine hata kubaini hali aliyonayo kisaikolojia. Lugha atumiayo mtu huweza kumtambulisha kama mpole, mkorofi, mgomvi, mshika dini, mwanasiasa, taahira wa akili au mlevi. Hii hutokana na ufundi au namna aitumiayo katika kufikisha ujumbe kwa wengine. Makala haya yamejiegemeza zaidi katika kipengele cha isimu saikolojia ambayo hutazama jinsi ubongo wa binadamu unavyohusiana na kuchakata lugha aitumiayo binadamu. Katika makala haya, tumeshughulika na kundi la watu wenye taahira ya akili kuonyesha jinsi waitumiavyo lugha. Makala haya yatumiwe kama kiwakilishi cha makundi mengine ya watu kama wanasiasa, watu wenye magonjwa yasiyotibika na waliokata tamaa ya kuishi, pamoja na watu washika dini sana, wenye misongo ya mawazo na wengineo. Matumizi ya lugha huchunguzwa kwa kuzingatia jinsi na hali mtu kisaikolojia.