MCHANGO WA MBINU ZA KUFUNZIA KATIKA KUIMARISHA UMILISI WA MWANAFUNZI KUHUSU VIPENGELE VYA SARUFI YA KISWAHILI NCHINI KENYA
Abstract
Lugha ya Kiswahili hufunzwa kama somo la lazima katika shule zote za msingi na upili nchini Kenya. Hii ni baada ya serikali ya Kenya kutambua jukumu muhimu linalotekelezwa na lugha hii. Wanafunzi wengi wa Kiswahili nchini Kenya hujifunza lugha hii kama lugha ya pili (kuanzia sasa L2). Ujifunzaji wowote wa L2 hufanikishwa kwa kupitia uwiano wa njia mbili kuu: ujifunzaji rasmi unaofanyika darasani na upataji lugha. Ufanisi katika ujifunzaji wa lugha darasani huweza kuathiriwa na mambo kama vile: mbinu za kufunzia wanazotumia walimu, hali ya kisaikolojia ya mwanafunzi, uwezo wake, vitabu vya kiada anavyotumia miongoni mwa mambo mengine. Katika makala haya tulilenga kutathmini mchango wa mbinu za kufunzia wanazotumia walimu wa shule za upili nchini Kenya katika kuimarisha umilisi wa mwanafunzi kuhusu vipengele vya kisarufi. Ufunzaji wa dhana ya kirai nomino (KN) ambayo ni kipengele kimojawapo cha sarufi ya Kiswahili ulitathminiwa. Njia zilizotumiwa kufunzia dhana hii zilichukuliwa kuwa kiwakilishi cha njia zilizotumiwa kufunzia dhana zinginezo za sarufi ya Kiswahili. Aidha, umilisi wa wanafunzi kuhusu dhana ya KN ulichukuliwa kuwakilisha umilisi wa wanafunzi kuhusu dhana zinginezo za sarufi ya Kiswahili. Mahitimisho tuliyoyatoa katika makala haya yalitokana na utafiti tulioufanya katika Kaunti ya Nyandarua nchini Kenya.