MAPITIO YA TAFITI KUHUSU LUGHA YA KUFUNDISHIA KWA KUZINGATIA SERA MPYA YA ELIMU ILIYOPENDEKEZWA NCHINI TANZANIA
Abstract
Suala la lugha ya kufundishia katika elimu ya sekondari nchini Tanzania limetafitiwa na kujadiliwa kuanzia miaka ya 1970 hadi 2000, lakini mjadala huo unazidi kuleta mabishano wakati huu tunapoelekea katika kile kinachoitwa na watu wa tabaka aali kuwa ni ' zama za utandawazi ' . Mabishano hayo yanahusu lugha ipi, kati ya Kiswahili au Kiingereza, inafaa kutumiwa kama lugha ya kufundishia kuanzia elimu ya sekondari hadi elimu ya juu nchini Tanzania. Mwaka 2009, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi (Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, 2009) ilipendekeza Sera mpya ya Elimu na Mafunzo inayotaka Kiingereza kiwe lugha ya kufundishia kuanzia elimu ya awali hadi elimu ya juu. Sera hii iliyopendekezwa inapingana na matokeo ya tafiti mbalimbali na haijali hali halisi ya lugha ilivyo katika jamii nchini Tanzania. Kwa sababu hiyo, imenipasa kupitia upya toleo la awali la makala hii (Qorro, 2008) na kupitia upya tafiti mbalimbali zilizofanywa kuhusu suala la lugha ya kufundishia kwa kuzingatia sera mpya ya elimu nchini Tanzania iliyopendekezwa mwaka 2009. Aidha, tutajadili njia zingine zilizopendekezwa na tafiti hizi katika kushughulikia tatizo la lugha ya kufundishia.