Ruwaza Zinazojitokeza kwenye Sinonimu za Mkopo katika Lugha ya Kiswahili
Abstract
Kila lugha hukopa maneno kutoka lugha ngeni moja au zaidi kila zinapotagusana na jamiilugha ngeni. Kwa hiyo, suala la ukopaji wa maneno si la lugha fulani mahususi bali ni la lugha zote. Lugha ya Kiswahili kama zilivyo lugha zingine, imekopa maneno kutoka lugha za kigeni kama Kiingereza, Kiarabu na Kireno. Ukopaji maneno katika lugha hutokana na sababu mbalimbali mojawapo ikiwa ni kasumba ya wazungumzaji kukopa maneno kutoka lugha za kigeni hata kama msamiati unaokopwa upo katika lugha husika au ulikwisha kukopwa kutoka lugha za kigeni (Kiango, 1999). Matokeo ya ukopaji huo ambao unatokana na kasumba, ni kuwa na maneno mawili au zaidi ya kigeni yanayorejelea dhana ileile. Kuwapo kwa maneno mawili au zaidi yanayorejelea dhana ileile katika lugha huibua sinonimu. Wataalamu kama Ullmann (1967) na Kitundu (2022) wanadai kuwa sinonimu katika lugha hazijakaa kivoloya bali hufuata ruwaza fulani kimatumizi. Lugha ya Kiswahili kama tulivyoeleza ina maneno mengi ya mkopo kutoka lugha za kigeni zaidi ya 13. Hivyo, upo uwezekano wa kuwa na maneno mawili au zaidi kutoka lugha ngeni mbili au zaidi yanayoelezea dhana ileile. Hata hivyo, suala hili bado si bayana katika lugha hii. Kwa hiyo, ipo haja ya kuchunguza zaidi suala hili. Kwa mantiki hiyo, makala haya yanachunguza ruwaza zinazojitokeza kwenye sinonimu za mkopo katika Kiswahili. Ili kufikia azma hiyo, data za makala haya zimekusanywa kutoka katika Kamusi ya Kiswahili Sanifu (2019) kwa kutumia mbinu ya uchambuzi wa matini na kutoka kwa watoataarifa kwa kutumia mbinu ya hojaji. Ukusanyaji na uchambuzi wa data za utafiti huu umeongozwa na Nadharia ya Vijenzi Semantiki pamoja na Nadharia ya Matumizi.
DOI: https://doi.org/10.56279/mulika.na43t1.1