Ujitokezaji wa Ruwaza ya Shujaa wa Kiafrika katika Kisakale cha Mukwavinyika wa Jamii ya Wahehe
Abstract
Makala haya yamechunguza ujitokezaji wa ruwaza ya shujaa wa Kiafrika katika Kisakale cha Mukwavinyika wa jamii ya Wahehe. Tafiti tangulizi zinaonesha kuwa tendi na hadithi nyingi za mashujaa duniani huwa na ruwaza fulani inayofanana na safari yao (mashujaa) hupitia karibu hatua zilezile. Suala hili linatupatia muundo wa msingi ambao ni wa kiulimwengu na wenye kutabirika. Hata hivyo, suala hilo limeibua maswali kama vile: je, kama ruwaza za mashujaa kote ulimwenguni zinafanana, jamii hizo zinafanana pia? Kama hazifanani, je, jamii zinazotofautiana katika nyanja mbalimbali za maisha zinawezaje kuwa na ruwaza za mashujaa zinazofanana kwa kila hali? Hivyo, kilichofanyika katika makala haya ni kubainisha ruwaza ya shujaa kama inavyojitokeza katika Kisakale cha Mukwavinyika ili kubaini umbile lake ni la namna gani. Katika kufanikisha hilo, makala haya yameongozwa na Nadharia ya Ruwaza ya Shujaa kwa mujibu wa Raglan (1934). Aidha, data zake zimekusanywa kwa njia ya usaili na uchambuzi matini kutoka katika kijiji cha Kalenga kilichopo mkoani Iringa. Makala haya yamebaini kuwa ruwaza ya shujaa iliyojitokeza katika Kisakale cha Mukwavinyika ina hatua 15 alizozipitia shujaa katika makuzi yake. Pia, imebainika kuwa mashujaa wa Kiafrika wana ruwaza zenye vipengele vinavyofanana na vinavyotofautiana na vya mashujaa wengine ulimwenguni.
DOI: https://doi.org/10.56279/mulika.na43t1.6