Sauti za Usimulizi Zilivyotumika Kutoa Mtazamo wa Kisiasa katika Hadithi Fupi Teule
Abstract
Mtazamo ni miongoni mwa vipengele vya usimulizi katika kazi za fasihi. Wahakiki, wachambuzi na watafiti wa kazi za fasihi wamejadili mtazamo kama kipengele cha fasihi kwa namna mbalimbali. Baadhi yao ni: Ferguson (1982), Monolov (2007) na Yirsaw (2016). Ferguson (1982) na Monolov (2007) wanadai kuwa kutokana na ubanifu wa hadithi fupi, mtazamo hasa wa wahusika hauelezwi bayana kutokana na matumizi ya nafsi ya kwanza au nafsi ya tatu. Naye Yirsaw (2016) anaeleza kuwa mtazamo katika usimulizi wa hadithi fupi uko bayana kupitia msimulizi. Mawazo ya wataalamu hawa yanakinzana. Hata hivyo, katika uhakiki wao waligusia kipengele cha mtazamo kiujumla pasi na kuhusisha masuala ya kisiasa, kijamii na kiuchumi, masuala ambayo yanahusishwa na mtazamo katika kazi za fasihi. Kutokana na hali hiyo, makala haya yanakusudia kuchunguza mtazamo kwa kujiegemeza katika nyanja mahususi. Hivyo, makala haya yamekusudia kuchambua sauti za usimulizi zilivyotumika kutoa mtazamo wa kisiasa katika hadithi fupi ya Shingo ya Mbunge ya Wamitila (2007) na Msomi Aliyebinafsishwa ya Nyangwine (2007). Makala haya yameongozwa na Nadharia ya Naratolojia ambayo imetupatia kile ambacho Bal (1997) anakiita “zana” ili kutusaidia kubaini na kufafanua sauti za usimulizi zilizotumika kutoa mtazamo wa kisiasa katika hadithi fupi za Shingo ya Mbunge na Msomi Aliyebinafsishwa.
DOI: https://doi.org/10.56279/mulika.na43t1.9