Makosa ya Kimofolojia ya Watumiaji wa Kiswahili na Sababu zake
Uchunguzi Kifani wa Watumiaji wa Kiswahili na Kihaya
Abstract
Watumiaji wa lugha ya Kiswahili wanapotumia lugha hiyo vibaya huibua makosa mbalimbali katika vipengele vya kiisimu. Makosa hayo yanaweza kuwa ya kifonolojia, kimofolojia, kisintaksia, kisemantiki au kipragmatiki. Makala haya yanachunguza makosa ya kimofolojia yanayofanywa na watumiaji wa lugha ya Kiswahili na sababu zake kwa kuhusisha watumiaji wa lugha ya Kiswahili na Kihaya. Data za msingi zilikusanywa uwandani kwa kutumia mbinu ya majadiliano katika vikundi lengwa na mbinu ya insha. Uchambuzi wa data za utafiti uliongozwa na Nadharia ya Usasanyuzi Dosari iliyoasisiwa na Corder (1967). Imebainika kuwa kuna makosa anuwai ya kimofolojia yanayofanywa na watumiaji wa lugha ya Kiswahili. Makosa hayo ni pamoja na kuongeza viambishi visivyohitajika kwenye neno, uchanganyaji msimbo, kutumia ngeli za nomino zisizo sahihi, kuhawilisha maumbo ya maneno ya Kiingereza katika Kiswahili na matumizi ya maumbo ya lughatandawazi. Pia, imebainika kwamba makosa hayo husababishwa na wazungumzaji kutojua vyema lugha ya Kiswahili, athari ya lugha ya Kihaya katika Kiswahili, tafsiri sisisi na ufanano wa kiumbo wa maneno ya Kiswahili na Kihaya. Aidha, makala haya yamebaini kwamba makosa hayo huleta athari mbalimbali kwa watumiaji wa lugha ya Kiswahili kama vile kushindwa kumudu ruwaza za lugha hiyo. Hivyo, watumiaji wa lugha ya Kiswahili na lugha nyingine, hawana budi kuacha ujumuishaji wa kuhawilisha maumbo yasiyo sahihi. Badala yake, wajifunze ngeli za nomino ili waweze kutumia maumbo sahihi ambayo yanakubalika katika lugha ya Kiswahili kwa azma kuzingatia sarufi ya lugha ya Kiswahili, utamaduni wa jamii na kuepuka kubananga lugha ya Kiswahili.
DOI: https://doi.org/10.56279/mulika.na43t2.3