Uchunguzi wa Mtagusano baina ya Hisia na Motifu
Mifano kutoka Tamthilia ya Ngoswe Penzi Kitovu cha Uzembe
Abstract
Motifu ni miongoni mwa vipengele vilivyochunguzwa kwenye matini za kifasihi andishi kwa mielekeo mbalimbali kama vile kuitumia kama nadharia ya uchambuzi na kama dhana ya uchambuzi. Licha ya tofauti za kimielekeo katika uchunguzi wa motifu, msingi wa tafiti hizo unatambua kuwa motifu ni kipengele radidi katika matini husika. Kwa kuwa matendo ya wahusika ndiyo yenye kuibua hali ya kujirudiarudia kwa jambo, kipengele cha wahusika kimeonekana kuhusishwa kwa karibu na motifu. Hata hivyo, ingawa tafiti na mawazo ya wataalamu hayahitilafiani kuhusu msingi wa utambuzi wa motifu, sababu inayochochea kujirudiarudia kwa vijenzi vinavyoijenga/vinavyoibua motifu hazipo bayana. Kwa hiyo, kwa kuzingatia mwelekeo wenye kuichambua motifu kama kijenzi tegemezi, utafiti huu ulifanyika ili kuchunguza vichocheo vyenye kukifanya kijenzi husika kijirudie kiasi cha kuibua motifu. Ili kutimiza lengo hilo, data zilikusanywa katika tamthilia ya Ngoswe: Penzi Kitovu cha Uzembe kwa kutumia mbinu ya usomaji matini huku uchambuzi wa data ukiongozwa na Nadharia ya Rasa. Matokeo ya utafiti yameonesha kwamba hali ya kujirudiarudia kwa jambo huchochewa na hisia za wahusika; hivyo, hisia na motifu hukamilishana.
DOI: https://doi.org/10.56279/mulika.na43t2.8