Urithi wa Vivuli
Kufichua Nyuzi za Baada ya Ukoloni katika Riwaya ya Nguu za Jadi
Abstract
Makala haya yanashughulikia urithi wa vivuli vya utawala wa kikoloni kwa kufichua nyuzi za baada ya ukoloni katika riwaya ya Nguu za Jadi iliyoandikwa na Clara Momanyi. Riwaya hii ilisomwa na mtafiti na baadaye masuala yaliyoonesha nyuzi za baada ya ukoloni yalidondolewa kwa kuzingatia lengo la makala haya. Lengo lenyewe lilikuwa kujadili jinsi ambavyo urithi wa vivuli huwekwa uchi kupitia nyuzi za baada ya ukoloni katika riwaya teule. Baadhi ya vivuli ni kama vile ukoloni mamboleo, ubaguzi, unyamazishaji, ufisadi, na uongozi mbaya. Kimsingi, makala haya yalichunguza namna madhara ya ukoloni yanavyoendelea kuathiri jamii baada ya kupata uhuru katika mfumo wa ukoloni mamboleo. Uchanganuzi wa makala haya uliongozwa na misingi ya Nadharia ya Baadaukoloni. Baadhi ya mihimili ya nadharia hii ni vita vya baada ya uhuru, ukoloni mamboleo, kuasi, na kutema. Uchanganuzi wa makala haya ulifanyika kwa kutumia mbinu ya kimaelezo. Njia kuu ya uchunguzi wa makala haya ilikuwa ya upekuzi-changanuzi wa yaliyomo. Ilibainika kuwa ubawa wa kibeberu ungali unayatawala mataifa ya ulimwengu wa tatu kupitia viongozi wa Afrika wanaotawaliwa na viongozi wa mataifa ya ulimwengu wa kwanza.
DOI: https://doi.org/10.56279/mulika.na43t2.9