Athari za Kifonolojia za Lugha ya Kwanza katika Kiswahili: Mfano wa Lugha Teule za Kibantu Nchini Kenya
Abstract
Lugha ya Kiswahili ina mfumo wa kifonolojia ambao una upekee unapolinganishwa na lugha nyinginezo. Ingawa hii ni lugha ya Kibantu, kunadhihirika tofauti anuwai tunapolinganisha muundo wa lugha hii na lugha nyingine za Kibantu katika kiwango cha kifonolojia. Tofauti hizi ndizo zinazosababisha athari za kifonolojia ambazo zinadhihirika katika matumizi ya Kiswahili na wazawa wa jamii mbalimbali za Kibantu. Makala hii inalenga kuweka wazi namna athari za kifonolojia zinavyodhihirika katika mawasiliano andishi ya Wabantu wanapoandika maneno mbalimbali ya Kiswahili. Aidha, njia sahihi ya kuyaandika maneno husika itasisitizwa. Data ya makala hii itatokana na uchanganuzi wa mawasiliano andishi ya wanafunzi wa shule za upili katika shule teule nchini Kenya. Utafiti huu ulifanywa katika wilaya ya Nakuru na ulihusisha wanafunzi 100 wa kidato cha tatu kutoka shule kumi teule. Mawasiliano husika yanahusu uandishi wa insha. Uchanganuzi unaovyaza data ya makala hii ulifanywa kwa kuzingatia Nadharia ya Uchanganuzi Makosa (Corder, 1967). Matokeo ya uchunguzi huu yatawasaidia wanafunzi wa taaluma ya Kiswahili kwa kuwa makosa yatakayochanganuliwa yatawawezesha kutofautisha kati ya Kiswahili sanifu na athari ya lugha mama katika Kiswahili. Kwa walimu wa Kiswahili, mifano ya makosa itakayochanganuliwa itakuwa hazina mahususi ya kuwawezesha kuwaelekeza wanafunzi wao kuhusu haja ya kuepuka makosa ya aina hiyo katika mawasiliano andishi. Uchanganuzi husika pia utasaidia katika kuimarisha uchunguzi kuhusu matumizi ya lugha ya Kiswahili, hususani kipengele cha uchanganuzi makosa.