Uhusika wa Mwanamke katika Nyimbo za Kizazi Kipya Tanzania
Abstract
Uhusika wa Mwanamke ni dhana iliyojadiliwa kwa mapana kupitia nyimbo za Kiswahili za muziki wa dansi, taarabu, dini na hata nyimbo za kizazi kipya kila wakati. Katika makala yetu, tumeonesha namna uhusika wa mwanamke ulivyosawiriwa katika nyimbo za kizazi kipya kwa kupitia maneno ya nyimbo za wasanii Ben Pol, Mwasiti Ft. Linnah, Zainab Lipangile, Barnaba Boy, Twenty Percent, Dayna Feat Marlaw, Vick Kamata, Nakaya Sumari, Diamond Platmamz, Lady Jay Dee, Jaguar Kenya, Ally Kiba na Banana Zoro. Katika uchambuzi wetu, tumeyanukuu baadhi ya maneno ya nyimbo hizo kwa lengo la kushadidia kile kinachozungumzwa juu ya uhusika wa mwanamke katika jamii inayomzunguka.
Tumetumia nadharia ya ufeministi, hususani ufeministi wa Kiafrika, katika kuyajadili matatizo anayokabiliana nayo mwanamke wa Kitanzania hususani katika kipengele cha udhalilishwaji, ukandamizwaji na udunishwaji wake. Aidha, makala yetu imeujadili uhusika wa mwanamke dhidi ya tabaka kandamizi katika jamii kwa kuijadili dhana ya mwanamke huyu na uhusika wake katika nyimbo za kizazi kipya. Makala imezipitia na kuzichambua nyimbo za Kiswahili za kizazi kipya. Mwishoni tumehitimisha na kupendekeza nini kifanyike ili kumkwamua mwanamke huyu.