Wahusika wa Kitashtiti katika Gamba la Nyoka
Abstract
Makala hii inachunguza uumbaji wa wahusika katika Gamba la Nyoka ambayo ni mojawapo ya riwaya za Euphrase Kezilahabi. Tumewatambulisha na kuwachunguza wahusika wakuu watano ambao ni Mambosasa, Mamboleo, Padri Madevu, Mama Tinda na Mzee Chilongo. Lengo letu ni kudhihirisha kwamba uumbaji wa wahusika hawa umetumia mtindo wa kitashtiti. Tashtiti ni mbinu pana inayojumuisha mbinu nyingine kadha (Wamitila, K.W. 2003:223). Hata hivyo, ili kuondoa uwezekano wa kukanganya, tunaweza kuzichukulia mbinu kama vile kinaya, ucheshi, dhihaka na bezo zinazotumiwa kuiunda kama vijenzi vyake. Kisawe cha istilahi tunayoizungumzia kwa lugha ya Kiingereza ni satire. Kwa vile tashtiti hudhamiriwa kukashifu na pia kupiga vita maovu ya kijamii, makala hii inaangazia matumizi ya mbinu hizi katika kufanikisha lengo hilo.