Muundo wa Utenzi wa Wabukusu wa Khuswala Kumuse
Abstract
Makala hii inashughulikia muundo wa Utenzi wa Khuswala Kumuse kwa kutumia Nadharia ya Umaumbo. Kulingana na Wafula na Njogu (2007), Umaumbo hulenga kuainisha sifa za kisanaa zinazopatikana katika fasihi kama taaluma. Wazo hili linaoana na maoni ya Njogu na Chimerah (2011) wanaoeleza kuwa katika fasihi kuna umbo la nje (kama vile sura, beti) na umbo la ndani (kama vile, jazanda). Umbo la shairi linategemea mpangilio wake. Kwa mfano, katika ushairi wa kimapokeo, yanapatikana mashairi yaitwayo tathlitha, tarbia na takhmisa, baina ya mengineyo kulingana na mishororo iliyomo katika kila ubeti. Kwa upande mwingine, ushairi wa kisasa hauzingatii sana umbo. Hata hivyo, shairi linaweza kuwa na beti fupi au ndefu; linaweza kuwa na umbo la kitendawili au ngano. Umbo ni namna kitu kilivyopangwa na kuundwa kwa nje na kwa ndani. Makala hii imedhihirisha ukweli wa madai haya kwa kuonesha kuwa kimuundo, Utenzi wa Khuswala Kumuse una mwanzo, kiwiliwili, upeo na hitimisho. Aidha, makala hii imeonesha kuwa utenzi unaorejelewa hauzingatii kaida ya idadi maalumu ya mishororo kwa kila ubeti wala idadi maalumu ya mizani kwa kila mshororo. Urari wa vina haupo. Utenzi huu pia hauna kibwagizo. Hata hivyo, utenzi huu ni mrefu kwani una beti zisizopungua tisini. Data ya makala hii ilitokana na uchunguzi wa maktabani. Hatimaye, mapendekezo ya utafiti wa baadaye yametolewa.