Kiswahili kama Chombo cha Kutangaza na Kuuza Vyombo vya Habari nchini Kenya
Abstract
Makala hii inatathmini ufaafu wa matumizi ya maneno ya Kiswahili kama anwani ya vituo vya redio vilivyochipuka katika miaka ya hivi karibuni nchini Kenya. Makala inaangalia jinsi ambavyo hali hii inaweza kuchangia uimarishaji wa lugha ya Kiswahili kwa jumla. Tangu azali na hata enzi ya ukoloni, lugha ya Kiswahili imekuwa zana muhimu ya mawasiliano timilifu sio tu katika ukanda wa Afrika Mashariki bali pia kwa umma mkubwa wa kimataifa. Matumizi ya Kiswahili katika shughuli mbalimbali za binadamu yamekuwa mhimili muhimu wa kukuza na kueneza lugha hii (Tuli, 1985). Katika kizazi cha kisasaleo, harakati za kiuchumi zimejifaragua kutoka biashara ya bidhaa na kujumuisha huduma mbalimbali ikiwemo habari. Kama huduma, habari imekuwa nguzo muhimu ya ufanisi. Dhima ya habari katika maendeleo ya dunia ya kisasaleo imeifanya kuwa huduma ambayo wateja wake wanaongezeka kila uchao. Hii ni hali mojawapo iliyochangia kuchipuka kwa vituo vingi vya redio vinavyoitwa vya Kiswahili ambavyo hutoa matangazo yao kwa Kiswahili. Makala hii inajikita katika kuangalia ufaafu na uamilifu wa majina au anwani na kaulimbiu zenye maneno ya Kiswahili kwa vituo vya redio vilivyoanzishwa na vyombo vya habari katika miaka ya hivi karibuni. Makala inaangalia matumizi ya maneno haya ya Kiswahili kutajia vituo vya redio sawa na mikakati ya kutoa mshawasha kwa wasikilizaji kuonea fahari vituo hivi na kuwateka ili waendelee kuvisikiliza. Kwa namna hii, lugha ya Kiswahili hujitokeza kuwa na uwezo wa kutanguliza, kutambulisha, kutangaza na kuuza vituo hivi kwa umma mkubwa wa wasikilizaji. Kadri wasikilizaji wanavyoendelea kusikiliza na kuchangia mijadala katika vituo hivi ndivyo vituo hivi vinavyoendelea kukubalika kuwa maarufu miongoni mwa wasikilizaji. Vivyo hivyo ndivyo lugha ya Kiswahili inavyoendelea kuimarika, kupanuka na kuenezwa na hivyo kuakisi mustakabali bora wa lugha ya Kiswahili.