Namna ya Kuimarisha Utamaduni wa Kusimulia Hadithi katika Jamii ya Wamasaaba nchini Uganda
Abstract
Kwa muda mrefu Wamasaaba wamekuwa wakishughulika na usimulizi wa hadithi kikamilifu katika jamii yao lakini siku hizi hawashughuliki tena na jambo hilo. Wengi wao hasa wale ambao ni wasomi hawaoni umuhimu wa kusimulia hadithi kwani huchukulia jambo hili kuwa la watu ambao hawajaelimika. Hivyo utafiti wetu umefanywa ili kufafanua mambo yanayorudisha nyuma usimulizi wa hadithi katika jamii yao na kupendekeza hatua ambazo zinaweza kuchukuliwa ili kuimarisha usimulizi wa hadithi katika jamii hiyo. Utafiti huu unakusudia kujibu maswali mawili: ni mambo gani ambayo yamefanya Wamasaaba wa Bududa wakose kuendeleza utamaduni wao wa kusimulia hadithi? Ni nini ambacho kinaweza kufanywa ili Wamasaaba waendeleze usimulizi wa hadithi katika jamii yao? Mtafiti alikumbuka miaka ya 1960 na 1970 ambapo wazazi walisimulia watoto wao hadithi akaona kwamba kuna mambo mengi sana ambayo watoto wa sasa wanayakosa. Alikumbuka jinsi alivyosimuliwa hadithi na babake alipokuwa mtoto. Mara kadhaa, mtafiti alimtembelea bibi mzaa mama ambaye pia alikuwa na kipawa cha kusimulia hadithi. Katika miaka ya 1970 kwenye shule za msingi, usimulizi wa hadithi pia uliratibiwa. Wakati huo watoto waliitwa mbele ya darasa mmoja baada ya mwingine na kusimulia hadithi katika lugha ya mama, yaani LuMasaaba. Wale walioshindwa waliadhibiwa. Haya ni mambo ambayo hayapo tena sasa ikilinganishwa na miaka ambayo imetajwa.