Uamilifu wa Mkazo katika Kiswahili Sanifu
Abstract
Mkazo ni hali ya neno au silabi katika neno kusikika kwa nguvu au kuwa na nguvu zaidi kuliko maneno au silabi nyingine (taz. Crystal, 1987:288; Massamba, 2004:52; Kihore, Massamba na Msanjila, 2008:28). Makala hii inahusu uamilifu wa mkazo katika Kiswahili sanifu. Kumekuwapo na mkanganyiko wa uamilifu wa kipambasautimkazo na vipambasauti vingine ambavyo ni kiimbo na kidatu katika Kiswahili sanifu. Mgullu (1996) anaelezea uamilifu wa mkazo juujuu lakini katika uelezaji wake anachanganya na uamilifu wa kiimbo. Hivyo makala hii imechunguza uamilifu wa mkazo katika Kiswahili sanifu ili kuondoa mkanganyiko huo. Tunapozungumza uamilifu wa mkazo tunarejelea dhima za mkazo. Uamilifu wa mkazo unajitokeza katika kiwango cha tungo neno na kiwango cha tungo kirai na sentensi. Hivyo, makala hii imeweza kubaini kuwa mkazo katika kiwango cha tungo neno na tungo kirai na sentensi kwa kawaida huwa na uamilifu wa kuwekewa nguvu katika silabi au neno wakati wa utamkaji. Ambapo huonesha msigano wa msikiko katika viambajengo vinavyohusika. Aidha, kuna wakati mkazo huwa na uamilifu wa kuonesha msisitizo katika kiambajengo kinachohusika yaani katika tungo neno au tungo kirai na sentensi. Hata hivyo, katika kiwango cha tungo neno ni mara chache sana mkazo unapohama husababisha maana ya msingi ya neno kubadilika. Hivyo, uamilifu wa mkazo umesaidia kubaini kuwa kipambasauti mkazo kina uamilifu tofauti na kipambasauti kiimbo na kidatu katika Kiswahili sanifu. Aidha, kuna mazingira mengine kiimbo na kidatu huweza kuathiri mkazo lakini licha ya athari hiyo ya kimsikiko haibadili uamilifu wa mkazo.