Nafasi ya Kiswahili kama Lugha Rasmi nchini Kenya: Majukumu na Changamoto

Authors

  • Jim Ontieri

Abstract

Kiswahili ndiyo lugha ya taifa nchini Kenya na kwa kiasi kikubwa inaeleweka na kutumiwa na Wakenya wengi kwa ajili ya mawasiliano ya kila siku. Ingawa kwa miaka mingi, lugha hii imetajwa kama lugha rasmi, hususani katika mawasiliano bungeni, katiba ya zamani haikuitambua kama lugha rasmi. Katiba mpya inakitambua Kiswahili kama lugha rasmi sambamba na Kiingereza. Hali hii inamaanisha kwamba, lugha hii imepewa majukumu mapya ya kimatumizi nchini Kenya. Kinyume na wakati ambapo lugha ya Kiswahili imekuwa ikipuuzwa na hata kuchukuliwa kama lugha ya wasio na elimu ya kisasa, lugha hii sasa imepewa hadhi katika jamii ya Wakenya wa matabaka mbalimbali. Ni wazi kuwa hali hii mpya itachangia pakubwa katika kutimizwa kwa ndoto ya wasomi wa Kiswahili na hata viongozi wa kisiasa barani Afrika ambao wamekuwa wakipendekeza kuwa Kiswahili kiwe lugha inayotumiwa katika shughuli rasmi kote barani Afrika. Kwa sasa Kiswahili ndiyo lugha rasmi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na imependekezwa kama lugha mojawapo ya Muungano wa Afrika (Momanyi, 2009). Kenya ikiwa nchi mojawapo iliyo na ukwasi mkubwa wa kimatumizi wa Kiswahili barani Afrika, ina nafasi ya kipekee ya kueneza matumizi ya lugha hii nchini na barani. Hili ni jambo ambalo kwa kweli limepewa msukumo mkubwa kutokana na Kiswahili kupewa hadhi ya lugha rasmi nchini Kenya. Suala kuu litakalowekwa wazi katika makala haya ni majukumu ya Kiswahili katika nyanja mbalimbali miongoni mwa wananchi wa Kenya. Aidha, changamoto anuwai zinazotarajiwa kuikumba lugha hii katika utekelezaji wa majukumu husika, zitajadiliwa.

 

Downloads

Published

2017-08-11

Issue

Section

Articles