Uainishaji wa Ushairi wa Kiswahili kwa Kutumia Kigezo cha Methali
Abstract
Makala haya yanahakiki methali kama mtindo unaotumiwa katika utunzi na uwasilishaji wa ushairi wa Kiswahili. Kwa mfano, hapo awali utungo huu ulitungwa kwa kuzingatia utamaduni wa Waswahili kama jamii. Kwa wakati wa sasa unatungwa na wasanii kutoka jamii pana ya Afrika Mashariki na kwingineko. Kipengele cha methali ni miongoni mwa kauli maarufu zinazotumiwa katika mashairi ya kimapokeo na mashairi huru ya Kiswahili. Aidha, baadhi ya wasanii wanawasilisha tungo zao kwa kuzingatia zaidi kauli mahususi wanazozibuni kwa makusudi au zile teule zinazopatikana katika mapokeo ya jamii. Katika muktadha huu, ushairi wa Kiswahili una sifa anuwai ambazo huweza kutumiwa kubainisha zaidi. Kuzingatia au kutozingatia kwa uwazi matumizi ya methali katika uwasilishaji, tungo hizo zinaweza kuainishwa kimakundi. Kwa hivyo, ushairi wa sasa wa Kiswahili unaweza kuwa ni ule unaozingatia methali zaidi, chache au ule unaoficha matumizi yake katika ujumbe au maudhui yanayowasilishwa.