Makuadi wa Soko Huria (Chachage S. Chachage) katika Muktadha wa Riwaya ya Kihistoria katika Fasihi ya Kiswahili
Abstract
Miongoni mwa kazi bora za fasihi duniani ni zile zilizojikita katika matukio na/au mashujaa halisi wa kihistoria. Mifano mizuri ni tendi za Homer za Kiyunani, baadhi ya tamthilia za W. Shakespeare (k.m. Julius Kaisari), na riwaya mashuhuri za Kirusi za Pushkin na Leo Tolstoi. Katika fasihi ya Kiswahili, riwaya ya kihistoria haijaendelezwa sana. Miongoni mwa kazi zilizoinua kiwango cha riwaya ya kihistoria katika Kiswahili ni Makuadi wa Soko Huria. Makala haya yataichambua riwaya hiyo katika muktadha wa riwaya ya kihistoria katika Kiswahili ili kuona mchango wa riwaya hiyo, na wa Chachage mwenyewe, katika kuuendeleza na kuukomaza mkondo huo wa uandishi wa kubuni.
_______________________________________
"Mtu huandika kitabu kimoja tu katika maisha yake."
Chachage S. Chachage
_______________________________________
" €¦katika kuandika historia isiyokuza ushujaa wa mtu au watu binafsi, Chachage amemkaribia mwandishi mashuhuri wa kimapinduzi, Maxim Gorky. Kwangu mimi, hili tu linatosha kumweka Chachage katika orodha ya wasanii stadi wa Tanzania, na wa Bara la Afrika" (Issa Shivji ,2002).