Uzingativu wa Vipengele vya Kimuundo kama Inavyoakisiwa katika Tafsiri za Awali katika Kiswahili na Lugha za Kibantu
Abstract
Mara nyingi nadharia za tafsiri zinasisitiza uzingatiaji wa maudhui katika matini huku zikitupilia mbali masuala ya kimuundo ambayo pia ni muhimu katika aina fulani za matini zinazotafsirwai. Tafsiri za awali katika Kiswahili na lugha za Kibantu nchini Tanzania zimeakisi suala la uzingatiaji na umuhimu wa vipengele vya kimuundo katika uhawilishaji wa maudhui ya matini husika. Tafsiri za awali hapa ina maana ya tafsiri zilizofanywa na wamisionari, wakoloni na baadhi ya wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili wakati wa ukoloni na kipindi kifupi baada ya uhuru. Makala haya yanakusudia kuchambua na kuainisha vipengele vilivyohawilishwa katika matini hizi kutoka katika matini za lugha chanzi. Aidha, yataonesha na kusisitiza umuhimu wa kuzingatia vipengele vya kimuundo katika tafsiri za aina mbalimbali za matini. Lengo la makala haya si kurejesha nyuma mjadala ambao umekuwepo kwa muda mrefu juu ya kipi muhimu kati ya maudhui au vipengele vya kimuundo katika tafsiri, bali ni kubainisha kwamba, pamoja na msisitizo mkubwa wa kuzingatia maudhui, vipengele vya kimuundo pia ni muhimu katika kufanikisha uhawilishaji wa maudhui hayo. Matini zitakazorejelewa ni matini za kifasihi, kidini na za masomo maalumu, hasa zilizotafsiriwa kabla ya miaka ya 1980 na wamisionari, wakoloni na baadhi ya wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili na lugha nyingine za Kibantu. Masuala yatakayochambuliwa ni pamoja na vipengele vya kisanaa, muundo na mtindo. Data itachambuliwa kwa kutumia mkabala wa ulinganishaji kati ya matini ya lugha chanzi na ile ya lugha lengwa.