Uchanganuzi wa Fani katika Kuakisi Dhamira za Kiteolojia katika Diwani Teule za Kiswahili

Authors

  • Eric Ndumbaro Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
  • Leonard Ilomo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
  • Joviet Bulaya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

Abstract

Makala haya yanachunguza jinsi vipengele vya kifani vinavyotumika kuwasilisha dhamira za kiteolojia katika ushairi andishi wa Kiswahili. Ingawa baadhi ya wanazuoni, mathalani, Trilling (2008), wanapinga kuwapo kwa uhusiano kati ya fasihi na teolojia, wakisisitiza kuwa fasihi haipaswi kuhusishwa na masuala ya kiteolojia, kuna hoja zinazopinga msimamo huo. Crosby (2022) anaeleza kuwa mitazamo ya kihistoria kuhusu teolojia na fasihi, hasa mwishoni mwa Zama za Kati, ilifanya baadhi ya watu, kutilia shaka ufanisi wa fasihi katika kueleza ukweli wa kiteolojia. Kutokana na mitazamo hiyo, kazi za waandishi kama vile Donne, Herbert, na Vaughan hazikutambuliwa kutokana na kuhusisha kazi zao na masuala ya teolojia (Calloway, 2023). Hata hivyo, Watson (2022) anakosoa mitazamo hiyo kwa kusema kuwa kuna kuchanganya kati ya teolojia na dini. Anaeleza kuwa teolojia ni taaluma inayojadili uhusiano kati ya nguvu kuu (kama Mungu) na viumbe, ilhali dini ni mfumo wa ibada na kujisalimisha kwa nguvu hizo. Teolojia, kwa hivyo, ni taaluma ya kiakademia inayochunguza imani, maadili, na maisha ya umilele. Katika kuchunguza dhihiriko la dhamira hizo, makala haya yamejikita katika diwani mbili: Wino wa Kalamu Ndogo (2019) na Ngonjera Zetu 1 (2020). Ili kufikia lengo hilo, makala yametumia mbinu ya usomaji makini na Nadharia ya Udhanaishi. Matokeo yanaonesha kuwa vipengele vya kifani kama taswira, muktadha, mtindo, na matumizi ya lugha vinatumika kuakisi dhamira za kiteolojia. Inapendekezwa tafiti zaidi zifanyike kwa lengo la  kulinganisha dhamira za kidini na kiteolojia ili kuelewa tofauti kati ya dhana hizo katika fasihi ya Kiswahili.

DOI: https://doi.org/10.56279/mulika.na44t1.3

Downloads

Download data is not yet available.

Downloads

Published

2025-06-30

Issue

Section

Articles