Mdhihiriko wa Kani ya Ardhi katika Riwaya Teule za Muhammed Said Abdulla
Uchanganuzi wa Kiontolojia
Abstract
Makala haya yanahusu mdhihiriko wa kani ya ardhi katika riwaya teule za Muhammed Said Abdulla kwa kuzingatia uchanganuzi wa kiontolojia. Ardhi ni kipengele cha kiontolojia chenye kani kubwa katika jamii za Kiafrika (Khamis, 2022). Inaaminika kuwa ardhi ina uhusiano wa moja kwa moja na maisha ya mwanadamu; yaani ina uwezo wa kuzalisha, kuendeleza na kumaliza uhai wa watu katika jamii husika (Hassan, 2018). Makala yametumia riwaya teule za Muhammed Said Abdulla kudhihirisha kuwapo kwa fikra kuhusu kani ya ardhi katika jamii za Kiafrika. Hivyo, hoja kuu ya makala haya ni kwamba katika riwaya teule za Muhammed Said Abdulla (kuanzia sasa MSA) kunadhihirika kani ya ardhi kiontolojia. Kani hizo zinapatikana katika maeneo, mapambo na matumizi yake. Makala haya yameongozwa na Nadharia ya Ontolojia ya Kiafrika. Data za makala haya zimepatikana maktabani. Mbinu iliyotumika kukusanyia data ni uchambuzi wa matini. Mjadala ulifanyika kwa kuegemea katika riwaya tatu za MSA ambazo ni Kisima cha Giningi (1958), Duniani Kuna Watu (1973) na Kosa la Bwana Msa (1984). Matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa ardhi ina kani kiontolojia kupitia vipengele vya maeneo na sifa zake, mapambo ya ardhi na matumizi ya ardhi.
DOI: https://doi.org/10.56279/mulika.na44t1.4